Friday, February 14, 2020

Kenya Yawatimua Wachina Wanne Kwa Kosa la Kumchapa Viboko Mkenya Aliyechelewa Kazini

Raia wanne wa china waliokamatwa na Mkurugenzi wa idara ya upelelezi wa makosa ya jinai (DCI) wanatarajiwa kurudishwa kwao baada ya amri iliyotolewa na Waziri wa mambo ya ndani wa Kenya Fred Matiang'i.

Agizo hilo lilisainiwa na Matiang'i Jumatano baada ya mahakama kuruhusu polisi kuwashikilia wachina wanne kwa siku 15 huku uchunguzi ukiendelea juu ya tukio la kumchapa viboko raia wa Kenya aliyekua akifanya kazi katika mgahawa ulioendeshwa na Wachina hao mjini Nairobi.

Raia hao wa china waliotambuliwa kwa majina; Ou Qiang, Deng Hailan, Chang Yueping, na Yu-Ling; walitiwa nguvuni Jumapili baada ya video iliyoonyesha mmoja wa wahudumu wa mgahawa wa wachina akipigwa viboko na mmoja wao katika mgahawa wao kueneo kwenye mitandao ya kijamii.

Katika video hiyo mwanaume wa Kichina alionekana akimpiga viboko Mkenya aliyekua akifanya kazi katika mgahawa unaouza vyakula vya kichina Chez Wou Restaurant katika eneo la Kileleshwa jijini Nairobi.

Iliripotiwa kuwa Mkenya, Simon Oseko, alikua akichapwa viboko kwa kosa la kuchelewa kufika kazini.

Alipigwa viboko viwili na meneja huku wafanyakazi wenzake wakishuhudia kwa mbali.

Oseko aliripoti tukio hilo katika kituo cha polisi. Iliripotiwa kuwa mpishi wa Kichina katika mgahawa huo pia aliwatisha wafanyakazi wengine raia wa Kenya ili wasizungumzie kuhusu mateso wanayopitia katika mgahawa.

Walikamatwa kwa kumiliki vibali vilivyopitwa na wakati vya kuishi nchini Kenya na kufanya kazi nchini humo bila kuwa na vibali vya kazi. Baadhi walikua na vibali vya kutembea Kenya
-BBC



Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...