Thursday, October 24, 2019

RC Sanare agiza Sokoine Memorial High School kupokea wanafunzi

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Loata Ole Sanare amewaagiza Afisa Elimu wa Mkoa huo na Viongozi wa Wilaya ya Mvomero na Halmashauri ya Wilaya hiyo kuhakikisha Sekondari ya Sokoine Memorial High School iliyopo Wilayani humo inapokea wanafunzi kwa ajili ya kuanza masomo mwaka huu bila kukosa.

Mkuu huyo wa Mkoa ametoa agizo hilo leo Oktoba 24 alipofanya ziara ya kuangalia utekelezaji wa Ujenzi wa mradi huo pamoja na majengo ya Mama na Mtoto yanayojengwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mvomero.

"miaka saba mradi unajengwa mmoja, sasa naomba tubadilishe staili, Mkurugenzi, lazima sasa hivi tuwachukue watoto sasa hawa wanaokuja, hakuna tena mjadala …….tuanze tufanye finishing (umaliziaji) wa majengo yale ya muhimu…tuanze sasa kuchukua watoto" amesisitiza Mkuu huyo wa Mkoa.

Ole Sanare amesema sio busara kusubiri fedha kiasi cha shilingi Bilioni 12 zinazohitajika kukamilisha ujenzi wa majengo hayo ndipo tuanze kuwapokea wanafunzi hao kwa ajili ya kuanza masomo bali fedha zilizobaki zaidi ya shilingi milioni mia moja zitumike kumalizia majengo yaliyopo mwishoni kumalizika ili wanafunzi waanze masomo mwaka huu.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wananchi wa Wilaya ya Mvomero kumpa ushirikiano ili kufanya kazi ya kuwaletea maendeleo wananchi Wilayani humo huku akiwaahidi kurudi tena ili kukaa nao na kujadili changamoto ya Migogoro ya Ardhi baina ya wakulima na wafugaji inayoendelea kujitokeza ili kuipatia ufumbuzi wa kudumu.

Hata hivyo amewataka wananchi wa Halmashauri hiyo kuishi kama ndugu na kujikita kwenye masuala ya maendeleo ikiwemo suala la Elimu badala ya kuendekeza Migogoro isiyo na tija kwao.

Awali akitembelea majengo yanayojengwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mvomero yatakayotoa huduma ya mama na Mtoto, Mhe. Ole Sanare aliwapongeza Viongozi wa Halmashauri hiyo kwa kusimamia fedha za Serikali zaidi ya shilingi 500 Mil.

Amesema katika mradi huo sio tu unakamilika kwa wakati lakini pia kwa kiwango bora kinachoendana na fedha zilizotolewa na Serikali.

Naye Mkuu wa Wilaya hiyo Mwl. Mohamed Utali pamoja na kupokea maagizo ya Mkuu huyo wa Mkoa alieleza sababu inayopelekea kiasi cha shilingi milioni mia moja kinachotakiwa kutumika katika kujenga njia ya kupita wagonjwa kutoka jengo moja hadi jingine (Walk way).

Akitoa taarifa ya ujenzi wa Sekondanri ya Sokoine Memorial High School, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mvomero Florent Kyombo amemueleza Mkuu wa Mkoa kuwa mradi huo awali ulitengewa fedha Bil. 12 lakini baada ya uamuzi wa Serikali wa Kutumia Force akaunti, mradi huo sasa utakamilisha ujenzi wake kwa shilingi Bil. 7 pekee.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...