Monday, October 28, 2019

RC MNYETI : WANANCHI DONGOBESH WAPOKEENI WAFANYAKAZI WA HALMASHAURI YA MBULU


Na Beatrice Mosses - Malunde 1 blog 
WANANCHI wa kata ya Dongobesh wilaya ya Mbulu mkoani Manyara wametakiwa kuwapokea na kuwakaribisha wafanyakazi wa halmashauri hiyo ambapo wanatarajia kuhamishia makao makuu ya halmashauri hiyo ndani ya wiki hii.

Kauli hiyo imetolewa juzi na mkuu wa mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti alipotembelea na kukagua jengo jipya la halmashauri ya wilaya ya Mbulu linalojengwa kwenye kata hiyo. 

Mnyeti alisema  ujio wa watumishi hao wa halmashauri kwenye kata ya Dongobesh utaleta mabadiliko ya haraka lakini pia mji utachangamka na maendeleo yataonekana kwa haraka zaidi. 

"Sasa nikuombe Mwenyekiti  uwahamasishe wananchi wa Dongobesh wawapokea watumishi kwa sababu tunaambiwa hapa kuna Ka Ukoo fulani ambako ndiko kana dominate kila kitu sasa kama mkifanya hivyo shauri yenu. 

"Lakini mkitaka maendeleo muwapokee watumishi, msiwafanye watumishi usiku wamelala wanaamka  wanajikuta wapo barabarani maana tunasikia kwamba hapa Dongobesh ni wataalamu sana wa sekta hiyo. 

"Niwaombe muwapokee watumishi na kuwafanya kama watoto wenu, sio tukileta hapa watumishi halafu mkawa mnawafanyia mambo ya namna hiyo tutawaondoa, tutajenga nyumba za halmashauri maeneo mengine watakuwa wanakuja kufanya kazi wanaondoka", Alieleza Mnyeti. 

Hata hivyo Mnyeti alishauri kwamba pindi watumishi wa halmashauri hiyo watakapohamia kwenye eneo hilo uitishwe mkutano wa wazee wa kimila wawapokee na kuwapa ulinzi wa kimila asidhurike mtu hata mmoja. 

Pamoja na hayo Mnyeti alipongeza kazi ya ujenzi unaoendelea kwenye jengo la halmashauri hiyo ambalo linajengwa na kampuni ya kijeshi ya Mzinga ambapo alidai kuwa fedha iliyotolewa inaendana na kazi inayofanyika. 

"Ingelikuwa tumetoa pesa halafu hakuna kinachofanyika tungesikitika sana, mwanzoni nilipita hapa nilimkuta mzee mmoja  tu na hapakuwa na mtu mwingine, nilisikitika sana   kwa sababu Mzinga tunaowaamini ni makampuni ya kijeshi ambayo tunaamini kwamba kazi zao zinakwenda kijeshi tulitoa mawazo yetu,  tulitoa ushauri na mmetekeleza tunawapongeza sana. 

"Sasa mlichonishawishi ni kitu kimoja tu kikubwa kwenda kuwatafutia pesa ili ije pesa nyingine muweze kuendelea na ujenzi huu na kwa spidi hii kwa kweli mmetufurahisha kwani hakuna kitu kibaya kama kuletewa pesa halafu miradi inakuwa haiendi",alisema.  

Kwa upande wake Mwenyekiti  wa halmashauri ya wilaya ya Mbulu Joseph Mandoo alipongeza kazi kubwa inayofanywa na Rais Magufuli kwa kusimamia fedha za watanzania kutokana na huko nyuma kutokuwa na historia nzuri. 

"Sisi wana Mbulu niseme ametupendelea sana kwa sababu ametupa miradi mikubwa ya maendeleo kwenye shule za sekondari na msingi lakini kubwa zaidi ni kutuletea fedha bilioni mbili na milioni Mia tano kwa ajili ya ujenzi wa jengo la halmashauri ya wilaya katika mji wa Dongobesh lakini pia ametuletea fedha zaidi ya bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya", alieleza Mandoo. 

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...