Monday, July 8, 2019

Waziri Lugola Apiga Marufuku Makamanda Wa Polisi Kuyakamata Mabasi Usiku, Asema Nchi Ina Amani, Ataka Yasafiri Saa 24 Bila Kubugudhiwa

Na Felix Mwagara, Mwibara (MOHA)
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amepiga marufuku Makamanda wa Polisi wa Mikoa nchini kuyazuia mabasi yanayotoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa kwenda Dar es a Salaam au kurudi Kanda ya Ziwa kusafiri muda wa usiku kwa kisingizio cha kuofia kuvamiwa na majambazi.

Lugola amesema Jeshi la Polisi lipo imara na kamwe haliwezi kucheka na majambazi wala kuwaonea huruma majambazi na kuanza kutupangia majambazi muda gani mabasi yasafiri na yasisafiri, mabasi hayo yanapaswa kusafiri saa 24.

Akizungumza na katika mkutano wa hadhara Kijiji cha Namibu Kata ya Neruma, Jimbo la Mwibara, Wilayani Bunda, Lugola amesema mabasi yanayosafiri kutoka Kanda ya Ziwa kwenda Dar es Salaam yasizuiwe Morogoro na yanayotoka Dar es Salaam kwenda kanda ya ziwa yasizuiwe Shinyanga kwasababu zinazodaiwa za kiusalama.

"Mimi ndiyo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, hatuwezi kupangiwa ratiba ya kusafiri na majambazi, Serikali ya Rais Magufuli ipo imara, na Polisi ipo imara, hivyo agizo hili ambalo pia niliwahi kulitoa lizingatiwe ipasavyo, niliagiza majambazi wote wasambaratishwe, asakwe mpaka jambazi wa mwisho, akamatwe kama kuku".Alisema Lugola na kuongeza.

"Taarifa ya uhalifu zinaonyesha Jeshi la Polisi limefanya kazi kubwa ya kupambana na uhalifu na hasa uhalifu wa majambazi, na niliwahi kuagiza kipindi hiki si cha kuwa na huruma na majambazi ni kipindi cha kuwashughulikia ili wananchi waishi kwa amani".

Lugola alifafanua kuwa, nchi haiwezi kupangiwa na majambazi muda wa kusafiri, kufanya biashara, hivyo maelekezo aliyoyatoa kwa Jeshi la Polisi liendelee kupambana na majambazi popote walipo nchini.

"Nimeelekeza magari yanayosafiri yasizuiwe Morogoro yanpopita muda wa usiku saa nne usiku na kuendelea, yasizuiwe Shinyanga, ili majambzi wajue popote walipo wapo imara wamejipanga vizuri na mimi Waziri wao nipo imara kuhakikisha Jeshi la Polisi linawashughulikia makambazi mmoja baada ya mwingine ili kuwafanya wananchi katika nchi yao waendelee kushughulika na masuala ya kujijengea uchumi ili Serikali ya Rais Magufuli, iweze kuwa na uchumi wa kati na majambazi wote wakamatwe kama kuku," alisema Lugola.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...