Friday, June 21, 2019

Serikali yapiga marufuku ufuta kuuzwa kwa walanguzi


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge amepiga marufuku wananchi kuuza ufuta kwa walanguzi badala yake wanatakiwa kuuza kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani.

Dk Mahenge alitoa agizo hilo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Keikei Tangini kata ya Keikei baada ya kusikia malalamiko kwa wananchi kuuza ufuta kwenye maghala kwa mtindo wa skakabadhi ghalani.

Pia alimuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto kupanga askari na kuhakikisha wanakagua magari yaliyobeba ufuta kabla haujauzwa kwenye minada kupitia kwenye maghala yasipite kwenda kuuzwa Dodoma mjini.

Pamoja na hayo alimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kondoa Vijijini, Yusufu Mgambo kuhakikisha anakusanya ufuta wa wananchi akiwa na uhakika wa kuwalipa ndani ya siku mbili badala ya kukusanya na kukaa nao bila kuwalipa.

Dk Mahenge alisema ufuta unatakiwa kuuzwa kwa mnada baada ya kuhifadhi kwenye maghala na wananchi ambao watakuwa wamelipwa fedha zao badala ya kuuza kwa walanguzi ambao wanaifanya pia halmashauri hiyo kukosa mapato.

Alisema mfumo huo wa stakabadhi ghalani ni agizo la serikali kupitia vyama vya ushirika kwa mikoa yote ambayo inazalisha ufuta Dodoma ikiwemo, hivyo ni vyema viongozi wakaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu ubora wa mfumo huo.

Dk Mahenge alisema mfumo wa stakabadhi ghalani umepima faida mikoa mingi hasa ya kusini kuhusu korosho, baada ya kunyonywa na walanguzi kwa muda mrefu waliweka zao ghalani wakauza kwa mnada kwa bei kubwa na wakapata pesa na hadi wakanywesha mbuzi soda.

Alisema viongozi wanatakiwa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia vyama vya ushirika kwamba mfumo wa stakabadhi ghalani ni mfumo bora ambao utawapa faida kubwa na hawapunjwa na walanguzi wanaowalalia bei.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...