Dodoma. Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi 'Sugu' amewataka wasanii wa muziki wa kizazi kipya Tanzania kutumia vipaji kufanya kazi nzuri na kuachana na tabia ya kusaka sifa mbaya kwa lengo la kukua kimuziki.
Sugu ametoa kauli hiyo jana Jumatatu Juni 3, 2019 baada ya kuulizwa na Mwananchi nini maoni yake kuhusu wasanii kuwa na tabia ya kutengeneza matukio ya aina mbalimbali na kuyatumia kama gia ya kuwafanya wajulikane, matukio ambayo wengi huwaweka katika wakati mgumu.
Sugu amesema uamuzi wake wa kutotaka kutengeneza sifa mbaya ndio umemfanya apate mafanikio, kuwa na marafiki wa kada mbalimbali na kuaminiwa na Chadema kilichompitisha kuwania ubunge mwaka 2010 na 2015.
"Wakati wetu kulikuwa na magazeti ya udaku ukionekana katika magazeti hayo basi unajiona wewe ndio mkali na unaweza."
"Binafsi sikuyapa kipaumbele magazeti hayo na haikunipunguzia kitu na ndio maana kwa sasa nina marafiki wengi mpaka viongozi wa dini," amesema Sugu.
Ameongeza,
"Kuna watu nadhani wasingeweza kuwa marafiki zangu kama ningetafuta sifa mbaya ili kukua kimuziki. Leo hii wapo wanaojisikia fahari kukiri wazi kuwa mimi ni rafiki yao."
Amesema msanii akiweza kutengeneza vyema jina lake kupitia muziki, atapata kipato zaidi katika mambo mengine ikiwemo biashara.
"Ukijulikana unaweza kuwekeza katika maeneo mengine. Yaani jina lako linakupa uwezo wa kufanya mambo mengi. Unamuona Diamond (Platnumz) anauza hadi karanga, hayo ni mafanikio," amesema.
Kuhusu wasanii wakongwe amesema, "Ninawashauri kama walifanya vitu katika mazingira nafuu hawakufanikiwa ni wakati umefika watazame maeneo mengine ya kufanya."
"Wakija niwashauri kuhusu muziki nitawaambia wasiache wafanye nyimbo kuwafurahisha mashabiki wao hata kama wamebaki 5,000 lakini wafanye mambo mengine kama wakati umeshapita."
Amesema,
"Wakati ukipita sio tu kuchoka katika sanaa, sio kushindwa kufanya muziki ni wakati tu unakuwa umepita. Wapo wanaosema mbona Jay Z anafanya muziki na anakaribia miaka 60. Wanatakiwa kutambua kila kitu na muda wake na kila mtu ana muda wake wa kufanya jambo."