Inatokea siku moja anakualika kwa ajili ya chakula cha mchana, baada ya mtoko huo, unajisikia kutoka naye kwa mara nyingine.
Kutoka kwenu mara kwa mara kwenda kupata chakula cha mchana, unagundua kwamba huyu bwana ni mtu mwenye kiwango cha juu ya usikivu, katika mazungumzo yenu anaonekana sana kwamba ni mwelewa na mwenye subira. Hana papara katika kuzungumza na mara nyingi huwa ni msikilizaji. Huyu unaweza kumwita rafiki ingawa ni wa jinsia tofauti, si dhambi kuwa na rafiki wa jinsia tofauti bali urafiki huo unapaswa kuwa na mipaka.
Kuna kitu wenzetu wazungu wanakiita Emotional infidelity , kwa tafsiri yangu naweza kusema ni hisia za usaliti katika mapenzi. Maana yake ni kwamba unaruhusu mtu mwingine wa jinsi tofauti azibe pengo la hisia ambalo lingetakiwa lizibwe na mpenzi wako au mume wako.
Wanawake ni viumbe wa hisia, wanapenda sana kusikilizwa, na wanapenda kuona wapenzi wao au waume wao wanawasikiliza. Inapotokea hitaji hilo halitekelezwi na mpenzi au mume wake, basi ni rahisi sana atakapotokea mtu mwingine ambaye bila kujua akamudu kuziba pengo hilo kuvutiwa naye na kuhitaji kuwa naye karibu mara kwa mara.
Zifuatazo ni dalili ambazo zitakuonyesha kwamba ukaribu wako na rafiki uliyenaaye (jinsia tofauti) utakupelekea kuisaliti ndoa yako:-
1. Unatamani sana kumuona ukiwa na shauku kubwa ya kuwa naye karibu na kutumia muda mwingi kuwa naye.
2. Unapokuwa naye unajikuta ukimweleza matatizo ya mahusiano yako na mpenzi wako au mumeo.
3. Unajikuta ukimgusa gusa wakati mkiongea au kufanya naye utani unaoweza kupeleka ujumbe tofauti kwake kwamba labda umevutiwa naye kimapenzi.
4. Unawasiliana naye kwanza kabla ya kuwasiliana na mpenzi wako au mumeo pale unapokabiliwa na jambo lolote lenye kutatiza na linalohitaji msaada wa haraka au ushauri.
5. Unajikuta ukiwaza jinsi gani ungekuwa na amani iwapo ungekuwa na uhusiano naye wa kimapenzi au ndoa.
6. Inawezekana ukawa unamzuingumzia sana kwa mwenzi wako au kwa marafiki zako, au inawezekana ukawa humzungumzii kabisaaa na kuficha urafiki wenu.
7. Unajitahidi sana kuficha urafiki wenu na kutomzunguimzia rafiki huyo kwa mwenzi wako kwa sababu unajua kwamba jambo hilo linaweza kukuletea balaa.
Kwa ujumla unapojikuta umempata rafiki wa jinsia tofauti na yako halafu ukahisi kulipukwa na moyo juu yake zikiwemo dalili nilizozitaja hapo juu, basi ujue uhusiano wako na mume au mpenzi wako uko mashakani. Usipokuwa makini utamsaliti.