Thursday, May 2, 2019

Maandalizi Ya Maadhimisho Ya 26 Ya Siku Ya Uhuru Wa Vyombo vya Habari Duniani Yapamba Moto Jijini Dodoma.

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Ikiwa kila ifikapo Mei 3,kwa kila mwaka Tanzania huungana na Mataifa mengine Duniani kuadhimisha siku ya vyombo vya habari Duniani,Maandalizi ya maadhimisho hayo yamepamba moto jijini Dodoma ambapo kitaifa yanafanyika hapa mkoani Dodoma.
 
Akizungumza     jijini Dodoma katika maandalizi hayo  Mwenyekiti wa kamati ya Maandalizi  Nevili Meena amesema Wameshirikisha wadau mbalimbali wa habari wakiwamo waandishi wa habari,wahariri ,wamiliki vya vyombo vya habari, maofisa wa Serikali pamoja na mashirika mbalimbali ya Kijamii na Kimataifa  hapa nchini.
 
Sanjari na hayo ,Meena amesema katika maadhimisho hayo kutakuwa na mada mbalimbali zinazohusu changamoto zinazoikabili tasnia ya habari hapa nchini.

Kwa upande wake, Mkuu wa kitengo cha habari shirika la Elimu ,Sayansi na utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) ,Nancy Kaizilege amesema Jumla  ya waandishi wa habari 1,307 waliuawa kati ya mwaka 1994 na 2018 wakati wakitekeleza majukumu yao ya kikazi katika nchi mbalimbali Duniani
 
"Tishio hili linafanya tuwe macho wakati wote, lazima tusimame pamoja, tushikamane ili kulinda uhuru wa kujieleza na usalama wa waandishi wa habari"alisema.
 
Alisema kuwa ripoti  hiyo iliyotolewa na UNESCO, inadai kuwa waandishi wa habari 99 waliuawa katika kipindi cha  mwaka 2018 wakitekeleza majukumu yao maeneo mbalimbali.
 
Amesema  kuwa mwaka huu maadhimisho ya mkutano wa kimataifa yameandaliwa  kwa pamoja na Serikali ya Ethiopia na Umoja wa Afrika huko Addis Ababa, kuanzia 2 hadi 3 Mei 2019.
 
Aidha ameongeza kuwa,mada ya Mwaka huu ya  maadhimisho ya  26  uhuru wa vyombo vya habari ni "Vyombo vya Habari kwa Demokrasia: Tasnia ya Habari na Uchaguzi katika Nyakati za Upotoshaji wa Taarifa"



Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...