Sunday, May 5, 2019

Anusurika kuuwawa na Simba


Na Ahmad Mmow, Lindi.

Mtu mmoja anayetambulika kwa jina la Kizito Matei (59), mkazi wa kijiji na kata ya Rutamba, tarafa ya Rondo, wilaya na mkoa wa Lindi. Juzi usiku alinusurika kuuwawa na kuliwa na Simba.

Imeelezwa kwamba Kizito ambaye alijeruhiwa kwenye tukio hilo na amelazwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Lindi( Sokoine) alikutwa na mkasa huo majira ya saa tano usiku katika kitongoji cha Namatili.

Mdogo wake Kizito anaetambulika kwa jina la Michael alisema Kizito alipokuwa anarudi nyumbani kwake toka matembezini alipoona giza ni nene, na maeneo hayo yanawanyama wakali aliamua kuingia na kulala kwenye kibanda cha mgahawa ambacho kilikuwa hakijagandikwa.

" Simba walikuwa wawili, walikuwa wanamfukuza mbwa. Walipofika kwenye kibanda waligundua kulikuwa na mtu.Kwakuwa kilikuwa hakijagandikwa walimuona. Ndipo mmoja alipotaka amchomoe baada ya kupenyeza mkono kwenye mojawapo ya matundu," alisema Michael.

Ndugu huyo wa Kizito alisema kutokana na kitendo cha Simba huyo kutaka kumchomoa kwa nguvu kaka yake, ndipo alipomjeruhi maeneo mbalimbali ya mwili, hasa mkononi.

Alipoulizwa kaka yake aliwezaje kuokoka na kunusurika kufa kwenye tukio  hilo. Alisema baada ya kuchomwa na makucha aliamka kutoka usingizi na kupiga kelele. Ndipo watu walipokwenda kwenye eneo la tukio. Jambo ambalo lilisababisha Simba hao wakimbie na kutokomea kusikojulikana.

Maelezo yote ya Michael yaliungwa mkono na Kizito mwenyewe ambae kwa mujibu wa mmoja wa maofisa waandamizi wa hospitali ya Sokoine, Dkt Ernest Mhando anaendelea kutibiwa na hali yake inaendelea vizuri.

Dkt Mhando alithibitisha kwamba Kizito alipokelewa katika hosipitali hiyo akiwa amejeruhiwa,hasa mkononi. Hata hivyo hali yake inaendelea vizuri na anaendelea kutibiwa.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...