Monday, April 29, 2019

Mwinyi Zahera Aitwa na Takukuru

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), imewataka wadau wote wa michezo akiwemo Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera kuwasilisha malalamiko yao licha ya taasisi hiyo kuwatuma maofisa wake kufuatilia yanayoendelea kwenye Ligi Kuu Bara.



Takukuru wametoa kauli hiyo kufuatia hivi sasa wadau wengi wa soka kulalamika juu ya uwepo wa rushwa michezoni katika kuzihujumu timu kwenye mechi za mwisho za Ligi Kuu Bara. Zahera mara kwa mara amekuwa akilalamika juu ya baadhi ya timu kutumia vibaya fedha zao katika kuzihujumu timu nyingine.



Akizungumza na Championi Jumamosi, Naibu Mkurugenzi wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo, alisema kuwa kwa upande wao tayari vijana wao wapo kazini kufuatilia kila kitu kinachotokea katika ligi kuu kupitia timu shiriki huku akiwataka wadau akiwemo Zahera kuwapelekea malalamiko yao ili waweze kuyafanyia kazi.



"Ni kweli hizo taarifa zimetufikia lakini kitu kinachotusikitisha sana kutoka kwa wananchi (wadau) ni kwamba mambo yanaongelewa na watu lakini wahusika wanaoguswa na hayo mambo hawaji kutupa taarifa kwa ufasaha yaani kutupa kamili, nini kimetokea, nani kafanya nini wakati gani na wapi.



"Sasa tuna taarifa lakini ni za kuungaunga mno, sisi tungependa hao watu wanaolalamika waje watueleze, nani kachukua rushwa, wakati gani na wapi, sisi tunaingia kazini yaani tupo tayari, tumepata habari nusunusu vijana wetu wemekwenda kufanya uchunguzi lakini inakuwa vyema kama tunapata taarifa ambazo zimejitosheleza kwa sababu inatusaidia kuanza na tatizo kuliko kusubiria," alisema Mbungo.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...