Tuesday, March 5, 2019

WANASAYANSI WATOBOA SIRI YA KUTIBU UKIMWI


Mtu mmoja huko Uingereza ambaye alikuwa ni muathirika wa UKIMWI, amekuwa mtu wa pili ulimwenguni kupona ugonjwa huo, baada ya kupandikizwa ujiuji katika mifupa 'bone marrow'.

Ikiwa ni takriban miaka mitatu imepita tangu awekewe cells za bone marrow za kipekee zenye uwezo wa kuzuia maambukizi ya HIV na kutumia dawa maalum, mtu huyo ameonesha kutokuwa na dalili zozote za kwamba aliwahi kuwa na HIV.

"Hakuna virusi ambavyo tunaweza viona, hatuwezi kuvipata", amesema Dkt. Ravindra Gupta, ambaye pia ni Profesa na mtaalamu wa masuala ya HIV aliyeongoza timu ya wanasayansi kutoa tiba hiyo ya utafiti.

Kutokana na hilo, Dkt Gupta amesema kwamba kesi hii ni uthibitiso tosha wa dhana kwamba ipo siku wanasayansi wataweza kupata tiba rasmi ya UKIMWI na kumaliza kabisa tatizo hili.

 Lakini haimaanishi kuwa wameshaipata tiba kwa sasa.

Mtu huyo kutoka Uingereza anakuwa wa pili ulimwenguni kupata tiba hiyo, baada ya kijana wa Marekani Timothy Brown, kufanyiwa tiba hiyo hiyo na kupona kabisa, huko nchini Ujerumani mwaka 2007.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), ugonjwa wa UKIMWI tayari umeshaua takriban watu milioni 35 duniani tangu ulipoanza katika miaka ya 1980s, na hadi kufikia mwaka 2017 takriban watu milioni 37 wanaishi na virusi vya ugonjwa huo, huku madaktari wakikesha kutafuta tiba kumaliza kabisa ugonjwa huo hatari.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...