Thursday, February 21, 2019

Mkuchika Atangaza Kiama Kwa Watumishi Waliotafuna Fedha za Miradi ya Maendeleo

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt. (Mst) George H. Mkuchika (Mb) ameahidi kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale waliotumia vibaya fedha za miradi ya maendeleo na kupelekea kutomalizika kwa miradi hiyo.

Kauli hiyo ameitoa wilayani Liwale wakati wa kikao kazi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale mkoani Lindi, kabla ya kutembelea utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na TASAF wilayani humo.

Mhe. Mkuchika amewataka watumishi wote wanaojijua kuhusika na ubadhirifu wa fedha za miradi ya maendeleo kuzirudisha mapema kabla majina yao hayajafikishwa ofisini kwake.

Mhe. Mkuchika amefafanua kuwa, Serikali imekuwa ikipeleka fedha za miradi ya maendeleo kila wilaya mkoani Lindi ili kutekeleza ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwezo zahanati, vituo vya afya, umwagiliaji na ujenzi wa barabara lakini fedha hizo zimeonekana kutumika vibaya kwani miradi haijamalizika lakini fedha zimeisha.

Mhe. Mkuchika ameainisha kuwa, taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Liwale inaonyesha Halmashauri hiyo inadaiwa takribani shilingi milioni 465 hivyo kupelekea kuzorota kwa uchumi wa Wilaya hiyo kutokana na makusanyo ya fedha kuishia kulipa madeni yanayotokana na matumizi mabaya ya fedha.

Mhe. Mkuchika amesema, amechoshwa na barua za malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusiana na matumizi mabaya ya fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya wilayani humo.

Aidha, Mhe. Mkuchika amewataka watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Liwale kuridhika na mishahara yao na kuacha kuomba rushwa kutoka kwa wananchi wanapohitaji huduma kwani kwa kufanya hivyo, kunawanyima wananchi haki yao ya kupata huduma.

Mhe. Mkuchika amefafanua kuwa rushwa ni adui wa haki na kutoa angalizo kuwa nchi ambazo rushwa imekithiri, mwenye haki ni mtu mwenye fedha kwa kuwa kila sehemu ataweza kushinda kwa kutoa fedha zake.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George H. Mkuchika (Mb) yuko katika ziara ya kikazi mkoani Lindi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi kwa umma,  ikiwa ni pamoja na kukagua na kujiridhisha na utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na TASAF mkoani humo.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...