Leo November 23, 2018 Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko wamepelekwa gereza la Segerea baada ya kufutiwa dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Hatua hiyo inatokana washtakiwa hao kukiuka masharti ya dhamana katika kesi ya uchochezi inayowakabili pamoja na Viongozi wengine saba wa chama hicho.
Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri ambapo amesema washtakiwa hao wamedharau amri za Mahakama kwa makusudi.
Kuhusu Mbowe, Hakimu Mashauri amesema kuna mkanganyiko kuhusu taarifa za kuumwa kwake kwani mdhamini wake alieleza kuwa November 8, 2018 aliugua ghafla na kupelekwa nje ya nchi akiwa mahututi, huku wakili wake akieleza kuwa alipelekwa Afrika Kusini kwa matibabu.
Kuhusu Matiko, Hakimu Mashauri amesema sababu alizozitoa mdhamini wake kwamba aliudhuria ziara ya Kibunge nchini Burundi si za msingi kwani nchi inaongozwa kwa sheria na sheria inamtaka mshtakiwa yoyote pamoja na Cheo chake alichonacho bado yupo sawa na watu wengine wanyonge.
Kutokana na hatua hiyo, Hakimu Mashauri amesema anawafutia dhamana washtakiwa hao, ambapo wamepelekwa gereza la Segerea ambapo watakaa huko hadi hapo rufaa yao itakaposikilizwa. Kesi imeahirishwa hadi December 6, 2018 kwa ajili ya kutajwa.
Hata hivyo, baada ya uamuzi huo wakili wa utetezi Peter Kibatala amesema kuwa wataukatia rufaa uamuzi huo katika Mahakama Kuu ya Tanzania.
Mbali na Mbowe, Matiko, washtakiwa wengine ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu Bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya, na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Vincent Mashinji.
Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari 1 na 16, 2018, Dar es Salaam.