Tuesday, September 25, 2018

Profesa Ibrahim Lipumba Ataja Sababu za Kung'atuka CUF


Mwenyekiti wa chama cha wananchi (CUF) anayetambulika na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba amesema yuko tayari kuachia madaraka ya chama hicho endapo atapatikana mtu mwenye sifa.


Mwenyekiti wa chama cha wananchi (CUF) anayetambulika na ofisi ya Msajili, Prof. Ibrahim Lipumba.

Amesema hayo leo Septemba 25, wakati akizungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa CUF inafuata demokrasia hivyo ikiwa kuna mwanachama hai mwenye sifa ajitokeze kuwania uenyekiti kwani muda ukifika wa uchaguzi hakuna sababu ya kung'ang'ania madaraka.

"Nitampisha atakayekuja kuwania nafasi ya uenyekiti ili mradi tu awe na sifa za uenyekiti na akubalike kwenye chama, sitokuwa na pingamizi lolote", amesema Lipumba.

Amesema mpaka sasa hakuna mtu aliyejitokeza kuwania uenyekiti wa chama hicho ambaye atapitishwa pia kuwa mgombea urais 2020.

Lipumba akizungumzia suala la Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif kutajwa kuitwa CHADEMA haitakidhuru chama hicho kwa sababu CUF bado inakubalika Zanzibar na kusisitiza kuwa chimbuko la CUF ni Zanzibar, hivyo CHADEMA hawawezi kuiua CUF Zanzibar.

Kwa zaidi ya miaka miwili sasa, Chama cha Wananchi (CUF) kipo kwenye mgogoro mkubwa wa kiutawala uliosababishwa na hatua ya Profesa Ibrahimu Lipumba kujiuzulu na baadaye kutengua uamuzi huo.

Profesa Lipumba alitangaza kujiuzulu uenyekiti, Agosti 5, 2015 lakini baada ya mwaka mmoja akatengua uamuzi huo na kutangaza kurejea katika wadhifa huo jambo ambalo limepingwa na baadhi ya wanachama wakiongozwa na Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...