Wanaume wawili wanaodaiwa kuwa ni majambazi wanaotuhumiwa kuvamia duka la dawa baridi katika kijiji cha Lyabukande halmashauri ya Shinyanga (Vijijini) wamefariki dunia baada ya kupigwa risasi na polisi baada ya majibizano ya risasi.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule tukio hilo limetokea jana Septemba 9,2018 saa tano na nusu usiku katika eneo la kichaka cha kata ya Mwawaza manispaa ya Shinyanga.
Aliwataja watu hao kuwa ni Juma Shija Elewa(39) mkazi wa Kitangili na Joseph Ndugali Tall (34) mkazi wa Sikonge mkoani Tabora ambao walijeruhiwa kwa kupigwa risasi na kufariki dunia wakiwa jiani kuelekea hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga.
"Chanzo cha tukio ni majambazi hao walipokuwa wanakwenda kuwaonyesha askari vielelezo na eneo ambalo majambazi wenzao wamejificha na baada ya kufika eneo hilo kukatokea majibizano ya risasi toka kwa majambazi waliokuwa wamejificha ndipo marehemu hao wakajeruhiwa kwa risasi",alieleza Kamanda Haule.
"Kwenye eneo la tukio kulipatikana silaha bastola isiyokuwa na namba ikiwa na risasi nne ndani ya magazine moja,vibuyu na vocha mbalimbali za mitandao ya simu na baadhi ya vocha zilipatikana nyumbani kwa Juma Shija Elewa baada kupekuliwa ambazo zote hizo ziliporwa kwenye duka la dawa baridi eneo la Lyabukande tarehe 6.9.2018",aliongeza.
Aidha alisema katika operesheni inayoendelea kwa kushirikiana na askari wa Mwanza,Septemba 9,2018 majira ya saa nane mchana eneo la Nyegezi-Mwanza,jambazi aliyefahamika kwa jina moja la Shaban aliwakimbia polisi na kutelekeza gari lenye namba za usajili T.820 AT aina ya Toyota Corona ambalo lilitumika katika tukio la unyang'anyi kijiji cha Lyabukande.
"Bado tunaendelea na msako kuwatafuta na kuwakamata majambazi wengine waliohusika katika majibizano ya risasi,na jambazi Shaban aliyetelekeza gari,miili ya marehemu imehifadhiwa chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga",alieleza Kamanda Haule.
Na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Bastola isiyokuwa na namba ikiwa na risasi nne ndani ya magazine moja na vibuyu walivyokutwa navyo majambazi
Vocha zilizokutwa eneo la tukio
Gari iliyotelekezwa na jambazi Shaban