Monday, September 17, 2018

KUHUSU LOWASSA KUSTAAFU SIASA BAADA YA CHADEMA KUSHINDWA MONDULI


Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa amekanusha taarifa zinazosambaa mtandaoni zikidai kuwa ametangaza kustaafu siasa kutokana na chama chake cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kupoteza jimbo la Monduli ambalo amewahi kuliongoza.

Lowassa amesema hana taarifa za matokeo ya uchaguzi wa Monduli kwa kuwa yuko safarini akitokea Arusha kuelekea Dar es salaam wala hajazungumza chochote kuhusiana na kustaafu siasa.

"Nani kasema maneno hayo? Mimi niko safarini sijapata 'document' yoyote kuhusu matokeo ya uchaguzi wala sijaongea popote", amesema Lowassa.

Mapema leo yaliibuka majadiliano kwenye mitandao ya kijamii yakihusisha baadhi ya viongozi pia akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda akidai kuwa amepata taarifa kuwa Mjumbe huyo wa kamati kuu ya CHADEMA amestaafu siasa.

"Eti nimesikia kuwa Mzee wetu ameamua kuachana kabisa na siasa. Mh Gambo naomba uhakika wa hizi taarifa kwa sababu wewe upo karibu na Monduli", ameandika Makonda.

Uchaguzi wa marudio katika majimbo ya Ukonga na Monduli umefanyika jana Septemba 16, ambapo aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Ubunge katika Jimbo la Monduli kupitia chama cha mapinduzi (CCM) Julius Kalanga amefanikiwa kutetea nafasi yake ya Ubunge wa Jimbo hilo kwa kupata ushindi wa kura 65,714 huku mpinzani wake Yonas Laizer wa (CHADEMA)akipata kura 3,187.

Chanzo- EATV
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...