Tuesday, August 28, 2018

JINSI WAZIRI MPANGO ALIVYOMSHUKIA MAKONDA KAMA MWEWE SAKATA LA MAKONTENA...ATAKA VIONGOZI WA SERIKALI WACHUJE MANENO


Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango (kushoto) akielezwa jambo na Ofisa Forodha Mfawidhi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wa Bandari ya Dar es Salaam, Stephano Mathias (kulia) kuhusu samani zilizopo kwenye moja ya makontena ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alipofanya ziara ya kukagua jana. Picha na Wizara ya Fedha 


Na Julius Mnganga, Mwananchi 

 Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amemshukia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuhusu sakata la mnada wa makontena 20 yaliyopo bandarini.


Makontena hayo yenye samani za ndani kama viti, meza na mbao za kuandikia yenye umiliki wa Makonda yanadaiwa kodi inayokadiriwa kuwa Sh1.2 bilioni.
Jumamosi iliyopita, makontena hayo yalikosa wanunuzi katika mnada kutokana na watu wengi kushindwa kufikia bei iliyotajwa.
Baada ya makontena hayo kutouzika, juzi Jumapili Makonda alitoa onyo kuwa mtu atakayenunua makontena hayo atamlaani yeye na uzao wake.
Huenda kauli hiyo ya Makonda ndiyo iliyomfanya Waziri Mpango jana kufanya ziara ya kushtukiza katika Bandari Kavu ya Dar es Salaam (DICD), kukagua makontena hayo na akatumia mwanya huo kutoa onyo kwa viongozi serikalini.
Baada ya kuyakagua makontena hayo jana alasiri, Waziri Mpango aliwataka viongozi serikalini kuchunga maneno yao na akawaomba wanaotaka kununua samani hizo wasiogope.
Dk Mpango alisema wanachokifanya ni kusimamia sheria za nchi ambazo hazichagui sura wala cheo cha mtu.
"Niliapa kutekeleza sheria za nchi na sheria za kodi. Katika usimamizi wa sheria hizi, kamishna zisimamie bila kuyumba. Piga mnada mara ya kwanza, ya pili na ya tatu kadri sheria inavyokuruhusu. Sheria inasema mzigo ulioagizwa kutoka nje hauna msamaha wa kodi. Hivyo, mchakato ulioanza kuutekeleza endeleeni nao," alisema Dk Mpango akimuelekeza kamishna wa Forodha, Ben Usaji.
Dk Mpango alisema, "Niwaombe viongozi wenzangu serikalini tuchuje maneno. Nawaomba Watanzania, anayetaka kuja kununua samani hizi asiogope, aje kununua. Haipendezi kusikia eti mtu atakayenunua samani hizi atapata laana, tena ya Mungu. Kwa nini tunahusisha Mungu kwenye vitu vya namna hii? Nawaomba Watanzania anayetaka kuja kununua samani hizi aje, hakuna cha laana wala nini."
"Kamishna piga mnada mara ya kwanza, ya pili, ya tatu kadri sheria inavyokuruhusu. Hata mimi ningekuwa na hela ningekuja kununua tuone hiyo laana inatoka wapi," alisema Waziri Mpango.
Kuhusu kauli ya Makonda kuwa samani hizo ni kwa ajili ya ofisi za walimu, Dk Mpango alisema Serikali inathamini mchango wao na inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha inaboresha mazingira yao ya kazi.
"Tuliapa kusimamia sheria. Sheria za kodi mimi ndiye mwenye dhamana hivyo niulizeni ni wajibu. Si sahihi hata kidogo kuingilia utaratibu ambao umebainishwa kisheria. Kamishna endelea kupiga mnada mpaka kieleweke," alisema.
Waziri Mpango alisema sheria haitoi msamaha kwa samani kutoka nje na kila anayeziagiza anapaswa kufahamu hilo.
"Nimejizuia sana kujibizana kwenye mitandao, hii si hulka yangu lakini haya ndiyo maelekezo ya Serikali," alisema Mpango.
Historia ya makontena
Sakata la makontena hayo lilianza baada ya tangazo la TRA lililochapishwa kwenye gazeti la Serikali la Daily News Mei 12, likiwataka wamiliki wa mali zilizokaa bandarini kwa zaidi ya siku 90 kujitokeza kuzilipia.
Tangazo hilo lilionyesha kuwa TRA inakusudia kufanya mnada wa wazi Juni kwa mizigo iliyokaa bandarini kwa muda mrefu bila kukombolewa, ikiwamo ya Paul Makonda.
Kwa mujibu wa tangazo hilo lililotolewa na Kaimu Kamishna wa Forodha na Ushuru wa TRA, Ben Asubisye, wamiliki walitakiwa kuitoa mizigo hiyo ndani ya siku 30 kuanzia siku ilipotangazwa.
Tangazo hilo lililokuwa na orodha ya makontena zaidi ya 800, jina la Paul Makonda lilijitokeza mara 20 akiwa mpokeaji wa makontena 20 yaliyopo katika bandari kavu ya DICD yakiwa na samani.
Ingawa hakukuwa na uthibitisho kuwa Makonda ndiye mwenye makontena hayo wakati huo, Februari 16 mkuu huyo wa mkoa alikaririwa katika mtandao wa gazeti la Serikali la HabariLeo kuwa alipokea makontena 20 yenye samani zitakazotumika katika ofisi za walimu zinazoendelea kujengwa. Mzigo huo ulikuwa sehemu ya shehena ya makontena 36.
Samani hizo za ofisini zilizokuwa na thamani ya Sh2 bilioni, zilitolewa na Watanzania wanaoishi Marekani wanaojulikana kama Six Region Diaspora Council.
Kauli za Makonda
Akizungumza na Mwananchi kwa simu juzi, Makonda alisema alishiriki ibada mjini Ngara mkoani Kagera kuhakikisha makontena hayo hayapati wateja kwa kuwa anaamini Mungu alimpa kwa ajili ya walimu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Mwananchi lilikuwa limempigia simu Makonda baada ya kuthibitisha kuwa ni makontena yake ili kujua jitihada anazochukua kuhakikisha hayauzwi na badala yake yanatolewa kwa walimu kama yalivyokusudiwa.
"Leo (juzi) nimekwenda katika ibada ya Jumapili katika Kanisa la Anglikana mjini Ngara, nimefanya ibada maalumu kuhakikisha makontena hayo hayapati wateja kwa kuwa naamini Mungu alinipa kwa ajili ya walimu wa mkoa wangu," alisema Makonda.
Alisema kupatikana kwa samani hizo ni jitihada zake binafsi za kuboresha mazingira ya kufanyia kazi walimu ikiwa ni kumuunga mkono Rais John Magufuli aliyeamua kutoa elimu bure kwa Watanzania na hasa watoto wa masikini.
"Rais alitambua umuhimu wa elimu ndiyo maana kama msaidizi wake sikuona sababu ya kukaa kimya wakati mazingira ya walimu si rafiki na kusubiri kuwalaumu pale watoto wanapofeli bila kufanyia kazi changamoto zao," alisema Makonda.
"Baada ya kuona jitihada za Rais katika sekta ya elimu, kwa kutoa elimu bure nami nikawaza kama msaidizi wake, nafanya nini kuunga mkono kazi nzuri anayoifanya Rais."
"Ndipo Mungu aliweka wazo lake ndani ya moyo wangu juu ya ujenzi wa ofisi za walimu kama sehemu ya kuboresha mazingira yao. Kwa utukufu wake Mungu, akaandaa watu wa kuchangia tena kutoka nje na ndani ya nchi," alisema Makonda.
Akitumia maneno ya vitabu vitakatifu, Makonda alisema utukufu wa Mungu umejidhihirisha kwa Watanzania kuchangia, wakiwemo askari wa Jeshi la Kujenga Taifa waliojitolea kujenga majengo; benki kwa kununua saruji; baadhi ya viwanda kutoa mabati na nondo na wengine kujitolea masinki, mabomba na taa.
Wasemavyo wadau
Akizungumzia uamuzi wa TRA na kilichosemwa na Makonda, mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Benson Bana alisema ifike wakati kila mtu au taasisi ifuate sheria zilizopo.
"Nawapongeza TRA kwa kusimamia sheria. Hili ni fundisho kwa watu wanaotaka kukiuka sheria zilizopo. Zipo hata taasisi za dini," alisema Dk Bana.
Alisema kilichozungumzwa na Makonda ni msimamo unaotokana na imani yake kama ambavyo mtu mwingine yeyote angeweza kulalamika baada ya mali yake kushikiliwa lakini Serikali haina imani.
Dk Bana alilitaka Bunge kuona umuhimu wa kufanya mabadiliko ya sheria ili kuwapa nafuu wanaochangia maendeleo ya Taifa.
"Nadhani Makonda alikuwa haelewi sheria zilizopo vinginevyo angewaomba waliomchangia fedha za kuondolea mzigo huo bandarini. Sheria ni msumeno ingawa zinapaswa kuwa rafiki kwa baadhi ya mambo kama mchango huu," alisema.
Mwanaharakati wa haki wa binadamu, Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema haipendezi kwa Mkristo kwenda kanisani kufanya ibada inayokiuka sheria za nchi.
Alisema kama Makonda anaona TRA wamekiuka sheria basi anapaswa kufuata utaratibu wa kawaida kudai haki yake. Alisema anaweza kwenda mahakamani kama TRA hawatamuelewa.
Alisema Makonda anapaswa kuwa mfano na hasa kwa vijana wanaompenda kwa kuonyesha utii wa sheria za nchi badala ya kulalamika.
Dk Kijo-Bisimba alisema kuna watu wengi vijijini ambao kwa kukiuka sheria mali zao huwa na sifa za kupigwa mnada, lakini wakiwa na sababu za msingi huwa wanajieleza kupata msamaha, hivyo Makonda anapaswa kuwatia moyo.
Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar, Profesa Haji Semboja alisema kabla ya uongozi, Makonda ni mtu kama walivyo wengine wenye umri mdogo wanaofanya mambo ambayo hayawezi kufanywa na wazee.
"Kwa vijana mambo mengi yanawezekana. Hii ingeshangaza kama haya yangesemwa na mzee kama mimi. Makonda hawezi kuongea kama Semboja," alisema.
Alisema kutokana na vijana wengi kushika nafasi za juu, ulimwengu unashuhudia aina tofauti ya utekelezaji wa majukumu na hata mawasiliano baina ya wenye madaraka na wananchi wanaowatumikia.
"Tunaona yanayofanywa na Rais (Donald) Trump wa Marekani. Kila siku anajaribu kuwasiliana na wananchi kwa namna tofauti. Hata hapa nyumbani tunao viongozi wengi vijana ambao wanafanya vitu ambavyo visingefanywa na wazee," alisema.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...