Sunday, August 10, 2025

Mama Manyara adaiwa kumuua mtoto wake kikatili kwa shoka.


Na John Walter Babati, Manyara

Wakazi wa Kitongoji cha Vituwey, Kijiji cha Ngoley, Kata ya Mwada wilayani Babati mkoani Manyara wameshtushwa na tukio la kikatili lililofanywa na mwanamke anayejulikana kwa jina la Mariam Mohamed, anayedaiwa kumuuua mtoto wake wa kumzaa wa kiume mwenye umri wa miaka 2.5 kwa kumtenganisha viungo vya mwili wake kwa kutumia shoka.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Vituwey, Jackson Mombo, amesema tukio hilo lililotokea majira ya saa nne asubuhi Agosti 8, 2025, limewaacha wananchi midomo wazi na kushindwa kuamini kilichotokea. 

Ameongeza kuwa ni muhimu jamii kuwa karibu na mtu yeyote anayeonyesha dalili za mawazo mazito au matatizo ya afya ya akili ili kuepusha madhila kama hayo.

Mashuhuda wamesema kuwa baada ya mauaji hayo, Mariam alipiga yowe akisema "jamani nisaidieni, nimemuua mwanangu", hali iliyowafanya majirani kukimbilia nyumbani kwake ambapo walipofika, walimkuta akiwa hajakimbia, huku mwili wa mtoto ukiwa juu ya godoro wanalolalia.

Baadhi ya majirani wamesema hawaamini kuwa mama huyo amefanya kitendo hicho kwa akili timamu, wakidhani huenda alikuwa na tatizo la afya ya akili.

Baba mkwe wa Mariam, Kimweri Juru, ameeleza kuwa aliwahi kumpa onyo mara kadhaa kuhusiana na tabia ya unywaji wa pombe, lakini hakutaka kusikia, na kwamba matokeo haya yanaweza kuwa ni sehemu ya madhara ya tabia hiyo.

Wakati tukio linatokea, mume wa Mariam hakuwepo nyumbani kwani usiku alikuwa akilinda mazao shambani dhidi ya wanyama waharibifu.

Jeshi la Polisi limefika eneo la tukio, kuchukua mwili wa marehemu na kumkamata Mariam kwa uchunguzi zaidi.

Tukio hili limeongeza hofu kwa wakazi wa Tarafa ya Mbugwe, kwani ni la pili ndani ya wiki moja, baada ya lile la kitongoji cha Mbugani, Kata ya Magugu, ambapo mwanaume alimuua jirani yake mbele ya watoto wake wawili wadogo kwa kumkatakata kwa panga.

Wakazi wanasema matukio haya ya mauaji miongoni mwa watu waliokuwa wakiheshimika na kuonekana wema, yanahitaji uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo chake na kuchukua hatua za kudhibiti hali hiyo.

Thursday, August 7, 2025

Vasco Mgimba aibuka mshindi kwenye kura za maoni Ludende

 



Aliyekuwa Diwani wa kata ya Ludende wilaya ya Ludewa mkoani Njombe Ndugu Vasco Weston Mgimba ameibuka mshindi wa kura za maoni za wajumbe wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kata hiyo kwa ajiri ya kupata ridhaa ya kuwa diwani.

Mgimba aliyekuwa akitetea nafasi hiyo ameibuka kidedea kwa kupata kura 382 akimshinda mpinzani wake Stephano Weston Luoga aliyepata kura 11 za wajumbe ikiwa katika kata hiyo ni wajumbe wawili pekee waliokuwa wakishindania nafasi hiyo.

Tuesday, July 29, 2025

Airtel Africa Yatangaza Matokeo Mazuri ya Robo ya Kwanza 2025


Airtel Africa imetangaza matokeo bora kwa robo ya kwanza iliyoishia Juni 30, 2025, ikionesha ongezeko la wateja wanaotumia huduma za intaneti na Airtel Money katika nchi mbalimbali za Afrika.

Afisa Mtendaji Mkuu, Sunil Taldar, amesisitiza kuwa mafanikio haya ni matokeo ya utekelezaji wa mkakati thabiti unaolenga kuboresha huduma kwa wateja na kuwekeza katika teknolojia mpya kama vile Airtel Spam Alert ili kuhakikisha usalama na kuimarisha imani ya mtandao.

"Tunaendelea kukuza ujumuishaji wa kifedha na kuunganisha jamii nyingi zaidi barani Afrika," amesema.

Airtel Africa imeshukuru wafanyakazi na wadau wote kwa mchango wao katika kuhakikisha ukuaji endelevu na huduma bora kwa wateja nchini Tanzania na kwingineko.

 

Sunday, July 27, 2025

RC Manyara awapiga marufuku viongozi kujilimbikizia mali


Na John Walter-Babati

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, amepiga marufuku viongozi na watumishi wa umma mkoani humo kujilimbikizia mali ambazo wanashindwa kuziendeleza, akieleza kuwa hali hiyo inaziba fursa kwa wananchi wengine kupata maendeleo.

Sendiga alitoa agizo hilo Julai 24, 2025, wakati wa hafla ya kumkabidhi mkandarasi eneo la ujenzi wa stendi ya mabasi, barabara za lami na mitaro katika stendi ya muda ya Makatanini, mjini Babati.

Amesema baadhi ya viongozi wamekuwa wakijipatia mali nyingi – zikiwemo vibanda – lakini wanashindwa kuviendeleza, hali inayokwamisha matumizi bora ya rasilimali zilizopo kwa manufaa ya jamii.

"Marufuku kujilimbikizia vibanda vitakavyojengwa katika stendi hii mpya. Kila mmoja apate kibanda kimoja ili kutoa nafasi kwa wengine, wale waliopo sasa kwenye stendi ya muda wapewe kipaumbele kwa gharama nafuu," alisisitiza.

Aidha, alibainisha kuwa kukamilika kwa stendi hiyo kutachangia kukuza uchumi wa wananchi wa Babati na kuondoa kero ya vumbi ambalo limekuwa likisababisha maradhi kwa watumiaji wa stendi hiyo kwa muda mrefu.

Kwa upande mwingine, Mkuu huyo wa Mkoa alimwagiza mkandarasi anayetekeleza mradi huo, kampuni ya Wesons Engineers, kuhakikisha hakuna visingizio vya kuchelewesha utekelezaji wa mradi huo na kwamba kazi ifanyike kwa ubora na ikamilike kwa wakati.

"Tunataka kuona thamani ya fedha kwenye kila senti, hakuna sababu ya kuchelewa au kutoa visingizio. Ujenzi uende kwa kasi na ubora unaotakiwa," alisema Sendiga.

Mradi huo unatarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miezi 15 kwa gharama ya shilingi bilioni 19.996, na unahusisha ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 4.7 pamoja na mitaro ya kupitisha maji yenye urefu wa kilomita 8.15.

Ujenzi wa stendi hiyo mpya unatarajiwa kuwa mkombozi mkubwa kwa sekta ya usafirishaji mjini Babati na kuchochea biashara kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati.

Wednesday, July 16, 2025

‎Mwenge wazindua daraja la watembea kwa miguu Tipri Mbulu. ‎


Na John Walter -Mbulu

Mradi wa ujenzi wa daraja la watembea kwa miguu Tipri lililoko kata ya Gehandu, halmashauri ya mji wa Mbulu, umeleta afueni kubwa kwa wananchi takribani 3,995, wakiwemo wanafunzi ambao sasa wanaweza kuhudhuria masomo bila usumbufu wakati wote wa mwaka.

‎Akisoma taarifa ya mradi huo wakati wa mapokezi ya Mwenge wa Uhuru, Meneja wa TARURA wilayani Mbulu, Mhandisi Nuru Hondo, amesema kabla ya kujengwa kwa daraja hili, wanafunzi walikuwa wanakwamishwa na mvua kwa takribani miezi saba kila mwaka, jambo lililoathiri mahudhurio na maendeleo yao kielimu.

‎Ameeleza kuwa daraja hilo kutokana na uimara wake linaweza kudumu kwa miaka 70.

‎Mwenge wa Uhuru umepokelewa wilayani Mbulu kwa ziara ya kukagua, kutembelea, kuzindua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi mbalimbali yenye thamani ya Shilingi bilioni 44, ikiwemo miradi ya afya, miundombinu ya barabara na miradi mingine ya maendeleo.

‎Miongoni mwa miradi hiyo ni daraja hili la Tipri, ambalo linaunganisha vijiji vya Tsawa na Tipri.

‎Kukosekana kwa daraja hilo kwa muda mrefu kulisababisha wananchi kupata changamoto kubwa katika kupata huduma muhimu, hasa wakati wa mvua ambapo mto huo ulikuwa unakuwa kikwazo kikubwa. Mradi huo umegharimu zaidi ya shilingi milioni 158.9.

‎Akizungumza kwenye eneo la mradi, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025, Ismail Ali Ussi, ameipongeza halmashauri ya mji wa Mbulu kwa ubunifu na utekelezaji wa mradi huu muhimu.

‎Vilevile, ameishukuru kamati ya ulinzi na usalama kwa usimamizi mzuri wa fedha za mradi.

‎Mwenge wa Uhuru mwaka huu unaendelea na kaulimbiu isemayo: ‎"Jitokeze kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa amani na utulivu."

Mwenge wa uhuru wazindua Mradi wa nishati mbadala Manyara Girls Sekondari



Na John Walter -Babati

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Ali Ussi, amezindua mradi wa nishati mbadala katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Manyara wenye thamani ya shilingi milioni 21.9.

‎Mradi huo unalenga kurahisisha upikaji wa chakula kwa wanafunzi pamoja na kutunza mazingira kwa kupunguza ukataji miti ovyo.

‎Kiongozi huyo amesema ni jitihada za Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya nchi na kulinda afya za Wananchi.

‎Akisoma taarifa kwa Kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru Kitaifa, Mkuu wa shule ya Manyara Girls, Bi. Gisella Msofe, amesema mradi huo wa gesi safi ya kupikia utapunguza muda wa kuandaa chakula na kuchangia jitihada za shule katika uhifadhi wa mazingira.

‎Baadhi ya wanafunzi akiwemo Sabrina Msangi, Faith Flavian na Sharon Msangi, wameishukuru serikali kwa mradi huo, wakieleza kuwa sasa watakuwa na muda zaidi wa kusoma badala ya kutumia muda mwingi kutafuta kuni, pamoja na kulinda afya zao kutokana na kupunguza moshi unaotokana na kuni na mkaa.

‎Mradi huo ni sehemu ya mpango wa serikali wa kuhamasisha wananchi kuachana na matumizi ya mkaa na kuni ili kulinda mazingira, ambapo serikali imeanza na taasisi zinazolisha watu kuanzia 100 na imekuwa ikitoa mitungi ya gesi kwa bei ya ruzuku ya shilingi 17,500.


Source

Gwajima: CCM Sihami, Tunabanana Mpaka Kieleweke



"Mimi bado ni mwanachama wa Chama cha Mapinduzi na nitaendelea kuwepo. Mimi sihami, CCM nipo sana, tunabanana humu humu ndani mpaka paeleweke pakae vizuri. CCM ni chama cha kidemokrasia kama ilivyo madhumuni ya katiba yake." - Askofu Josephat Gwajima


Tuesday, July 15, 2025

Mchambuzi Hans Rafael Amchana MO Dewji Vibaya: Asitufanye Sisi Watoto

 

Mchambuzi Hans Rafael Amchana MO Dewji Vibaya: Asitufanye Sisi Watoto


Binafsi nimemsikiliza Tajiri ila sıjaona utofauti wa kile alichoongea msimu uliopita na leo.

1. Mo anasema ametoa zaidi ya Tsh 80b,inawezekana ni kweli Ila atwambie na Yeye Simba imemtengenezea kiasi gani?….maana kila mwaka anatumia Brand ya Simba kutangaza bidhaa zake.


2. Mo amesema kila mwaka anatoa hela ya usajili ila mambo yamezidi kuwa yale yale kila mwaka Simba wanasajili Wachezaji 17 na mwisho wa Msimu wanakata 14 je Mo haoni pale Simba kuna shida ya utendaji? Kwani asiwaondoe viongozi wote wanaosajili…..? na kuajiri watu wapya wa mpira kama (Technical Director na Drector of football) ili wasimamie vizuri project na Pesa zake? Kwanini ameendelea kuwakumbatia viongozi wale wale ambao kila msimu wanafuja pesa zake kwa kusajili Wachezaji wa kawaida?


Binafsi nadhani hakuna tajiri mjinga ambae kila mwaka atakubali kupoteza hela Yake Kama hapati faida……Mo amekomaa na Simba coz anapata faida,biashara zake zinaenda,Simba ni Brand kubwa ambayo kila tajiri nchini anatamani kuitumia leo asitufanye sisi kama watoto😄


Ifike Muda matamko yakome,vitendo viongee,Simba kabla ya kupata hela ya Mo wanahitaji mfumo mpya wa katiba na viongozi Ila hawa wa Sasa sioni wakifanya Jambo

Mo Dewji : Toka Mwaka 2018 Hadi Leo Nimetumia Bilioni 87 Kwa Ajili ya Simba



"Kuanzia mwaka 2018 hadi leo nimewekeza shilingi Bilioni 45 kwa ajili ya mishahara, usajili, maandalizi ya Timu na mahitaji mengine ya uendeshaji, pia nimechangia shilingi Bilioni 20 kama sehemu ya ununuzi wa hisa asilimia 49 ndani ya Simba Sports Club na mara nyingi nimekuwa nikitoa msaada nje ya mfumo rasmi, kila palipojitokeza uhitaji wa dharura kuanzia mwaka 2017 hadi 2024 nimetumia takribani Bilioni 22 katika misaada ya dharura hivyo kufanya jumla ya mchango wangu kwa Simba kufikia shilingi Bilioni 87 hivyo kusema Mo hatoe hela ni kauli ya kupotosha yenye mwelekeo wa chuki, tuachane na fitna zisizo na msingi, tujenge palipotoboka, tuzibe ufa panapovuja na tusonge mbele bila kuonyeshana vidole" 

——— 
Mohammed Dewji, Mwekezaji na Rais wa heshima wa Simba Sports Club.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...