Saturday, January 31, 2026

Bilioni 24.9 kupeleka umeme vitongoji 218 Mkoani Njombe,REA Wamtambulisha Mkandarasi



📍Njombe

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan, ameelekeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kufikisha umeme kwenye vitongoji vyote vilivyobakia nchini ambavyo bado havina huduma ya umeme ifikapo mwaka 2030.

Hayo yamebainishwa leo Januari 30, 2026 na Frank Mugogo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mha.Hassan Saidy wakati wa hafla fupi ya kumtambulisha mkandarasi kutoka kampuni ya Central Electricals International Ltd katika Mradi wa HEP 2B ambaye anaenda kutekeleza kwenye vitongoji 218 mkoani Njombe.

"Jumla ya vitongoji vyote mkoa wa Njombe ni 1,833 na vitongoji vyenye umeme ni 1,276. Vilevile vitongoji ambavyo havina umeme ni 557. Hivyo mradi huu unakwenda kupeleka umeme kwenye vitongoji 218 katika mkoa huu na vitabakia vitongoji 339 ambavyo havina umeme navyo vitakamilika, " Amesema Mugogo.

Ameongeza kuwa, gharama za kuunganisha umeme huo ni shilingi 27,000 tu na kuwataka wananchi wa mkoa huo kutumia fursa ya kuunganisha umeme kwa gharama nafuu iliyowezeshwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe.Rais Samia.

Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo mkoani Njombe, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa Bw. Lewisi Mnyambwa amemshukuru Rais Samia kwa kuleta fedha nyingi zaidi ya bilioni 24 ili kupeleka umeme kwenye vitongoji vya mkoa wa Njombe.

"Serikali kupitia REA imefanya kazi kubwa. Tunasisitiza miradi hii ikamilike kwa muda uliopangwa na tutaendelea kuusimamia ipasavyo ili mkandarasi aweze kutekeleza majukumu yake pasipo changamoto yeyote katika kipindi chote cha utekelezaji wa mradi," Amesema Mnyambwa. 

Aidha, ametoa rai kwa wananchi wanaozunguka eneo la mradi kumpatia ushirikiano mkandarasi huyo na ametakiwa kutoa kipaumbele cha ajira kwa wazawa ili kufanya shughuli mbalimbali katika mradi huo ili uchumi wa wananchi uongezeke na wanufaike na uwepo wa miradi hiyo katika mazingira yao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miradi kutoka kampuni ya Central Electricals International Ltd, Bw. Zameer Meghji ameishukuru Serikali kupitia REA kwa kupewa fursa ya kutekeleza mradi huo mkubwa. Amesema watahakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati, watashirikiana na wananchi na kutoa kipaumbele cha ajira kwa wazawa ili miradi hiyo ilete tija kwa wananchi na nchi kwa ujumla.


Friday, January 16, 2026

MUUNGANO WAZIDI KUIMARISHA USHIRIKIANO NA KUIBUA VIPAJI VYA MICHEZO

Wachezaji wa Timu ya Mpira wa Pete (Netiboli) ya Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na (Mazingira) wakiwa katika picha ya pamoja muda mfupi baada ya kuwasili katika Uwanja wa Amani Complex, Zanzibar kwa ajili ya uzinduzi rasmi wa Mashindano ya Ligi ya Muungano ya Mchezo Pete (Netiboli) iliyozinduliwa leo Alhamisi Januari 15, 2026.

******************

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema itahakikisha uwepo wa Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar unaendelea kuimarika sambamba na kuibua fursa za ajira kupitia nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya michezo.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi (Januari 15, 2026) na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Ali Abdulgulam Ali wakati alipokuwa akizindua Ligi ya Taifa ya Muungano katika Uwanja wa Amani Complex, Zanzibar.

Mhe. Abdulgulam amesema michezo ni fursa ya ajira kwa vijana wa na hivyo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zitahakikisha zinatumia fursa hizo kuibua vipaji kwa vijana na kuwatengeneza ajira.

"Mashindano haya ni sehemu ya matunda ya Muungano uliojengwa kwa misingi umoja, amani na mshikamano….Serikali zote mbili zitahakikisha zinatumia fursa ya mashindano haya kuwezesha vijana kujitengenezea fursa za ajira" amesema Mhe. AbdulGulam.

Aidha amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itahakikisha inaendelea kushirikiana na Chama cha Netiboli Zanzibar (CHANETA) na Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA)katika kuratibu mashindano hayo ili kuwa nguzo muhimu katika kukuza umoja, upendo na mshikamano kwa Watanzania.

Ameongeza kuwa Serikali zote mbili ztaendelea kuweka mazingira wezeshi kupitia sekta ya michezo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya kisasa katika viwanja mbalimbali hatua inayolenga kuibua vipaji kwa vijana na kutengeneza ajira kwa Kundi hilo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Bi. Hanifa Selengiu amesema Serikali zote mbili zimeanzisha mashindano hayo kwa aijli ya kuhakikisha Watanzania wanaendelea kufahamishwa umuhimu wa Muungano na fursa zinazoibuliwa zilizopo ikiwemo sekta ya michezo.

"Mashindano ni utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyotoa mwaka 2024 kuhusu jukumu ilioipatia Ofisi ya Makamu wa Rais ya kuutangaza Muungano" amesema Selengu.

Amesema Michezo ni sehemu muhimu ya Muungano na hivyo mashindano hayo yamekuja katika wakati mwafaka hususani katika kipindi hiki ambacho Serikali imekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu kwa umma kuhusu Muungano kwa makundi mbalimbali ikiwemo vijana.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Zanzibar (CHANEZA) Bi. Nasra Juma amesema mashindano hayo yameshirikisha jumla ya timu 11 ikiwemo timu sita (06)kutoka Tanzania Bara na tano (05) kutoka Zanzibar.

Amezitaja timu hizo kuwa ni Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Uhamiaji, Tamisemi, Kikosi cha Kujitolea Zanzibar (KVZ), Afya- Zanzibar, Jeshi la Zimamoto, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mbweni, Taasisi ya Uhasibu Arusha (IAA), Polisi Dodoma, Mafunzo na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU).

Amesema Chama hizo kimeendelea kuweka mikakati mbalimbali katika kuhakikisha Ligi ya ya Netiboli ya Muungano itaendelea kupata washiriki wengi zaidi kwani mchezo huo kwa sasa umezidi kukua na kuweza kufungua milango ya fursa za ajira kwa vijana.

Katika michezo iliyochezwa mapema leo asubuhi Timu ya JKU iliwezesha kupata ushindi wa magoli 36 kwa 34 dhidi ya Polisi Arusha wakati Mafunzo Zanzibar iliiadhibu Timu ya Afya Zanzibar kwa magoli 79 kwa 24.
Watendaji Waandamizi wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira)wakifuatilia matukio mbalimbali ya hafla ya uzinduzi Mashindano ya Ligi ya Muungano ya Pete iliyozinduliwa leo Alhamisi Januari 15, 2026. Aliyesimama ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Muungano Ofisi ya Makamu wa Rais Zanzibar, Bi. Shumbana Taufiq.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Muungano Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Bi. Hanifa Selengu akiwasilisha salamu za Uongozi wa Ofisi hiyo wakati wa hafla ya uzinduzi wa mashindano ya Ligi ya Muungano ya Mchezo wa Pete (Netiboli) iliyozinduliwa leo Alhamisi Januari 15, 2026.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Muungano Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Bi. Cecilia Nkwamu akifuatilia matukio mbalimbali ya hafla ya uzinduzi wa Mashindano ya Ligi ya Muungano ya Mchezo wa Pete (Netiboli)yaliyozinduliwa leo Alhamisi Januari 15, 2026.

Wachezaji wa Timu ya Mpira wa Pete (Netiboli) ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) wakipita mbele ya Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Ali Abdulgulam Hussein muda mfupi kabla ya kuzinduliwa kwa wa Mashindano ya Ligi ya Muungano ya Mchezo wa Pete (Netiboli) iliyozinduliwa leo Alhamisi Januari 15, 2026.
Wachezaji wa Timu ya Mpira wa Pete (Netiboli) ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) wakipita mbele ya Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Ali Abdulgulam Hussein muda mfupi kabla ya kuzinduliwa kwa wa Mashindano ya Ligi ya Muungano ya Mchezo wa Pete (Netiboli) iliyozinduliwa leo Alhamisi Januari 15, 2026.
Wachezaji wa Timu ya Mpira wa Pete (Netiboli) ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) wakiingia katika wa ndani wa Amani Complex, Zanzibar kwa ajili ya kwa ajili ya uzinduzi rasmi wa Mashindano ya Ligi ya Muungano ya Mchezo wa Pete (Netiboli) iliyozinduliwa leo Alhamisi Januari 15, 2026.
Wachezaji wa Timu ya Mpira wa Pete (Netiboli) ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) wakiwa pamoja na wachezaji wa Timu mbalimbali zinazoshiriki mashindano ya Ligi ya Muungano ya Mchezo wa Pete (Netiboli)iliyozinduliwa leo Alhamisi Januari 15, 2026.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...