![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjb17iVR2knXOKRyLM_hEY19x7VleoCMw3SsLtzarDQJj8GzilwUN2VWDArz6_i51T45ggI-oJ_bmABioBd4tipPeeNXc5rUNILp3McMim4dgRiTu5xJ8J0lVXFjGwhcTKK3JhUzO3H_WCufIWibU_yjazW-daCN30mSWEQYiBQSiVIxZ2P6UR_QvAAJzur/w640-h358/1002135005.jpg)
Na Hadija Bagasha -Tanga
MKUU wa Mkoa wa Tanga Balozi,Dkt Batilda Burian amesema wameanza mazungumzo na hazina kuangalia uwezekano kwa waliopewa Viwanda na kuvitelekeza kuwanyang'anya ili wapewe watu wenye uwezo wa kuviendeleza na sio kuacha magofu.
Balozi Batilda ameyasema hayo wakati akizungumza na Viongozi wa dini na Viongozi wa vyama vya Siasa Mkoani Tanga ambapo amesema Mkoa huo umeanza mchakato wa kuvifufua viwanda vilivyokufa na hawataki kuona magofu.
Balozi Dkt Batilda amesema Tanga kulikuwa na Viwanda vingi ambavyo vilikuwa vinafanya kazi ikiwemo kiwanda cha Nondo,Msumari, Mbao na foma viwanda ambavyo watu walivichukua na kivitelekeza.
"Kulikuwa na kiwanda cha misumari hapa watu wamekichukua na kukitelekeza kulikuwa na kiwanda cha Nondo, mbao na Foma vyote hivyo kwa Sasa tupo kwenye mazungumzo na hazina kuangalia uwezekano waliopewa hivyo viwanda wanyang'anywe na wapewe watu wengine mabenki yapo vijana wapo BBT ya mama Samia Jenga kesho iliyobora ni pamoja na kuwawezesha vijana waingie Kwenye Uwekezaji, mifugo,uvuvi, kilimo hata viwanda mashine ambazo zinatengeneza misumari haizidi dola 30,000 na vijana watatengeza misumari wakaendesha kiwanda chao na Uchumi ukakua "Alisisitiza Balozi Batilda.
Aidha katika kikao hicho Mkuu huyo wa Mkoa wa Tanga amewataka viongozi wa dini katika mahubiri yao wahamasishe waumini kuhakikisha wanajitokeza kujiandikisha Kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ikiwemo kuboresha taarifa zao.
Dkt Batilda pamoja na mambo mengine alisema zoezi la uboreshaji wa Daftari la kura litaanza February 13 mwaka huu mpaka February 19.
Alisema ni upo umuhimu Mkubwa viongozi hao kutumia majukwaa yao kuhakikisha wanawaelimisha waumini juu ya umuhimu wa kujiandikisha katika zoezi hilo muhimu ili kupata haki ya kuwachagua viongozi katika uchaguzi mkuu mwaka huu.
"Ndugu zangu viongozi wa dini naombeni mtumie mahubiri yenu kuhakikisha mnawahamasisha wananchi kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga kura siku zimefika kesho tutakuwa na siku ya uandikishaji daftari "Alisema Batilda.
"Hivyo kupitia Tume Huru ya uchaguzi walikuja na kufanya semina na viongozi wa vyama na mafunzo kwa wataalamu na Jumuiya ngazi za Kaya na Mawakala na kesho tunakwenda kwenye zoezi la uandikishaji wale vijana waliofika miaka 17 ambapo ikifika mwezi Octoba watafikisha miaka 18 wanapaswa kujitokeza kujiandikisha"Alisema