
Na Regina Ndumbaro Masasi.
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara, limepitisha Rasimu ya Mpango na Bajeti ya Tsh 47,850,929,593 kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwa ni ongezeko la asilimia 10.3 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka uliopita.
Ongezeko hili limejumuisha pia ukuaji wa mapato ya ndani kwa asilimia 16.8, hatua inayolenga kuboresha huduma na miradi ya maendeleo katika wilaya hiyo.
Miongoni mwa vipaumbele vya bajeti hiyo ni kuanzisha na kuendeleza miradi ya kimkakati inayolenga kuongeza mapato ya halmashauri, ikiwemo ujenzi wa ghala la mazao mchanganyiko katika kata za Chigugu na Chiungutwa. Aidha, halmashauri inapanga kununua lori moja kwa ajili ya usafirishaji wa vifaa na malighafi za miradi ya maendeleo ili kuhakikisha utekelezaji wa miradi unakuwa wa haraka na wenye tija.
Katika sekta ya mawasiliano na jamii bajeti hiyo imeweka mkakati wa kuanzisha Redio ya Jamii ya Masasi ili kuongeza uhamasishaji na utoaji wa habari kwa wananchi
Pia kwa lengo la kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao, vituo viwili vya polisi vitajengwa katika kata za Chiwale na Mbuyuni, hatua ambayo inatarajiwa kupunguza matukio ya uhalifu katika maeneo hayo.
Sekta ya afya imepewa kipaumbele kwa kukamilisha ujenzi wa vituo vya afya viwili katika vijiji vya Chikundi na Chikoropola, pamoja na zahanati mbili katika vijiji vya Mbangala na Liloya.
Uwekezaji huu unalenga kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Masasi, hasa wale waliopo maeneo ya vijijini.
Katika sekta ya elimu, halmashauri imepanga kukamilisha vyumba vya madarasa 56, nyumba tatu za walimu, na vyumba vinne vya maabara ili kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
Hatua hii inalenga kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani na kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora katika mazingira yanayofaa.
Kuhusu ajira bajeti hiyo inajumuisha mpango wa kuajiri watumishi wapya 604 katika sekta mbalimbali, ikiwa ni hatua ya kukabiliana na uhaba wa watumishi uliosababishwa na kuongezeka kwa vituo vya kutolea huduma pamoja na kustaafu kwa baadhi ya watumishi wa umma.
Ajira hizi zitahusisha kada za afya (175), elimu msingi (214), elimu sekondari (76), uhasibu wasaidizi (3), kilimo (12), mifugo (7), ujenzi (3), na utawala (43).
Katika hotuba yake,Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Ndg. Later J. Kanoni, ameliomba Baraza la Madiwani kuhakikisha linajenga kituo kidogo cha polisi katika makao makuu ya halmashauri yaliyopo Mbuyuni ili kuimarisha usalama wa wananchi na mali zao.
Alisisitiza kuwa uwepo wa kituo hicho utasaidia kupunguza vitendo vya uhalifu na kuboresha mazingira ya kiusalama katika wilaya hiyo.




