Waandishi wa Habari wametakiwa kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na Chanjo ya Kipindupindu ili ipate uwelewa zaidi na kujua muhimu wa chanjo hiyo.
Akifungua Mafunzo kwa Waandishi wa habari Mkurugenzi Mkuu kutoka Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Dk Abdallah Ali Suleiman amesema lengo la mafunzo hayo ni kutoa elimu kwa jamii ili kuondokana na dhana potofu zinazotokana na chanjo hiyo
Amesema chanjo hiyo haina madhara yoyote kwa binadamu iko salama ambayo inatolewa kwa ajili ya kuikinga jamii na maradhi ya mripuko hivyo ameitaka jamii kuondoa shaka hiyo.
Ameeleza kuwa Chanjo ya Kipindupindu inatarajiwa kutolewa mwezi ujao katika shehia mbali mbali za Unguja na Pemba kwa maeneo ambayo huathirika sana kila unapotokea mripuko wa maradhi hayo.
Nae Afisa Afya ya Jamii Bi Faiza Mohamed Abdulkadir amesema chanjo hiyo inatarajiwa kutolewa kuanzia umri wa mwaka mmoja na kuendelea pamoja na wagonjwa wenye maradhi sugu yasiyoambukizwa ikiwemo presha sukari na mengineyo.
"Chanjo hiyo haitopaswa kupewa wagonjwa mahatuti na mama wajawazito na watoto chini ya mwaka mmoja", alifahamisha Afisa huyo.
Kwa upande wake Mratibu wa Chanjo kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) Dr. Vendelin Simon amesema kuwa chanjo iko salama tayari imeshatolewa katika nchi mbalimbali na haijaleta madhara yoyote kwa waliotumia ambayo ni dawa ya kunywa sio sindano hivyo ameisihi jamii kuwa na mwamko wa kushiriki kupata chanjo hiyo.
Zoezi la utoaji wa Chanjo ya kipindupindu linatarajiwa kufikia zaidi ya watu laki 3 (300,000) katika Wilaya tisa za Unguja na Pemba ikiwa jumla ya shehia 58 lenye lengo la kutoa kinga kwa wananchi katika kipindi cha miaka mitatu hadi mitano mpaka kumaliza dozi hiyo .