Mkazi wa mtaa wa Itumbi katika mji mdogo wa Makongolosi, Pantaleo Terespholi (30) amehukumiwa na mahakama ya hakimu mkazi Wilaya ya Chunya kifungo cha maisha jela na kuchapwa viboko 10 atakapoanza kutumikia adhabu hiyo baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka mtoto wa miaka mitatu.
Akisoma hukumu hiyo leo Ijumaa Februari 5, 2021 hakimu mwandamizi mfawidhi, Osmund Ngatunga mbele ya mwendesha mashtaka wa Serikali, Fredrick Ndosy imesema mshtakiwa alitenda kosa hilo Mesi mosi, 2020 katika eneo ya uchimbaji wa madini ya dhahabu kwa kumbaka mtoto huyo ambaye mama yake alikuwa anafanya biashara ya kuuza chakula.
Amesema mahakama imethibitisha bila shaka kutoka kwa mashahidi wanne kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo.
Amesema miongoni mwa mashahidi ni mama wa mtoto huyo, Anna Yohana aliyeeleza kuwa siku ya tukio wakati anauza chakula mtoto wake alitoweka saa 11 jioni na kutoa taarifa ambapo mmiliki wa mgodi huo na wafanyakazi wengine walisitisha shughuli zao na kuanza kumtafuta.
Hakimu amesema Anna alibainisha kuwa walimkuta mtuhumiwa akiwa kichakani bila nguo huku akiwa na mtoto huyo na tayari alikuwa amembaka, na alikamatwa na kupelekwa ofisi ya Serikali ya mtaa.
Aliwataja mashahidi wengine kuwa ni Dk John Francis aliyempokea Anna alipofika hospitali, shahidi wa tatu alikuwa askari polisi F 3661 D/ CPL Mohamed na shahidi na wanne ni mchimbaji mdogo wa aliyekuwepo wakati mtoto huyo alipotoweka na alimshuhudia mtuhumiwa kichakani.