MABINGWA wa kihistoria Tanzania, Yanga wamesema kuwa wapo tayari kumlipa mchezaji wao wa zamani Amiss Tambwe ambaye anawadai fedha za usajili pamoja na mshahara wakati akitumika ndani ya kikosi hicho.
Tambwe alikuwa ni mshambuliaji na pia aliwahi kucheza kwa watani zao wa jadi Simba kabla ya kuachwa na kuibukia ndani ya kikosi cha Yanga kinachonolewa na Kocha Mkuu, Cedric Kaze.
FIFA ilitangaza kuifungia Yanga kwa kile kilichotajwa kutomlipa mshambuliaji huyo madai yake ya Sh milioni 44 yaliyotokana na usajili wake.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela, alisema kuwa mashabiki wasiwe na hofu juu ya hukumu hiyo ya FIFA, wamejipanga vema kufanikisha hilo na wataendelea kufanya usajili kama kawaida.
"Mashabiki wa Yanga wasiwe na wasiwasi kabisa hizo milioni 44 tutazilipa haraka iwezekanavyo, tulivyoingia madarakani tulikuta madeni mengi katika timu, hivi sasa tumeyalipa na tunaendelea kuyalipa," alisema Mwakalebela.
Alipotafutwa Tambwe kuzungumzia hilo, alisema: "Hiyo adhabu waliyoitoa FIFA ni kweli, lakini kama watalizilipa hizo fedha wataruhusiwa kuendelea na usajili kama kawaida, ".