Friday, January 15, 2021

Waziri Ndugulile awataka wakuu wa Taasisi zilizochini yake kuwa wabunifu ili kuleta mafanikio na kuwa na tija


Na Ezekiel Mtonyole - Dodoma.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari  Dkt. Faustine Ndugulile amewataka watendaji wa taasisi zilizochini ya Wizara yake kuja na mikakati itakayowezesha taasisi hizo kupiga hatua na kuwa na mafanikio ya haraka na ndani ya siku 100 mikakati hiyo ionekane ya namna ya kuboresha huduma zao.                        

Dkt.Ndugulile ameyabainisha hayo Jijini Dodoma wakati wa kikao kazi cha kujadili utendaji kazi wa shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL kilichowakutanisha watendaji wa shirika hilo.

Amesema anataka ndani ya siku 100 kuona mambo makubwa yakifanywa ndani ya taasisi za Wizara yake ili kukidhi matarajio ya watanzania katika Wizara hiyo mpya.

"Hakuna kulala hizi siku 100, zikifika tu siku 90 tunataka matokeo yanayopimika na mtendaji wa kila taasisi atakuja mbele yangu kueleza ndani ya kipindi hicho imefanya nini,kinachopimika sio michakato,"amesema Dkt Ndugulile.

Ameongeza kuwa "Inawezekana siku za nyuma hamkuwa na mikataba Kindamba(Mkurugenzi wa TTCL) utakuwa na mkataba na mimi wa performance, utakuja kuniambia nini unakusudia kufanya, nikikubana wewe na wewe utaenda kubanana na wenzako,"amesema.

Sambamba na hilo, ameagiza Shirika la Mawasiliano Tanzania(TTCL) kuhakikisha wanapunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuweka mikakati ya kujiendesha kibiashara ili kukidhi soko la ushindani huku bidhaa zao zikipatikana kwa urahisi.

"Kumekuwepo na malalamiko kwa wananchi kama suala la upatikanaji wa vocha baadhi ya mikoa, vocha hazipatikaniki shida ipo wapi?, pia angalieni vifurushi vyenu, nyie mna advantage kuliko kampuni nyingine boresheni vifurushi vyenu,kitengo cha huduma kwa wateja pia kiboreshwe," amesisitiza.

Dkt Ndugulile ameongeza kuwa "Mje na mikakati ambayo ni mizuri tunajua mnamahitaji ya fedha lakini mje na mikakati inayopimika ili hata nikikupa Sh.Milioni 100 basi baada ya muda uniletee Sh.Milioni 300, lengo la Wizara ni kuona TTCL isimame sio kwa kubebwa bebwa kuweni na ubunifu,"alisema.

Akizungumzia matumizi, Dk.Ndugulile  amesema matumizi yao hayalingani na wanachokipata na kuwataka kuboresha huduma kwa wateja.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba amesema kwa miaka mitano kabla ya mwaka wa fedha 2016/17 shirika hilo lilikuwa likijiendesha kwa hasara ya Sh.Bilioni 15 kwa mwaka lakini tangu kuingia serikali ya awamu ya tano madarakani linajiendesha kwa faida ya sh. Bilioni 5 kwa mwaka.

Amesema Shirika hilo lipo mbioni kukamilisha mikataba miwili mikubwa ya utoaji huduma nchini Dubai na Malawi.

"Tunatarajia ndani ya siku 90 kufunga mkataba na kampuni kutoka Dubai wa Dola za Marekani zaidi ya Milioni 3.6 tatu, pia mkataba mwingine Malawi wa Dola za Marekani Milioni 3.2, tunataka kufanya ubunifu ndani ya muda uliotupa," amesema.

 

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...