Wednesday, January 20, 2021

Miili ya watu wawili waliozama kwenye maji Babati, yapatikana leo


Na John Walter-Manyara

Jeshi la Zimamotto na uokoaji mkoani Manyara limefanikiwa kuopoa miili ya watu wawili waliokuwa wamezama maji siku ya jumatatu jioni katika eneo la maporomoko ya maji (Tururu) yanayotoka mto Mrara mjini Babati.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Manyara Julishaeli Mfinanga akithibitisha tukio hilo, amesema watu hao walifika akatiika eneo hilo la Tururu kwa ajili ya kufanya utalii wa ndani kwa kuogelea na kupiga picha.

Kamanda Mfinanga amewataja waliofariki ni Joseph Isdori (19) na Abubakari Hamisi (21)  wote wakazi wa mtaa wa Negamsi Mjini Babati. 

Inaelezwa kuwa Joseph Isdori ni mhitimu wa kidato cha nne mwaka 2020 na amefanikiwa kufaulu kujiunga na kidato cha tano.

Shuhuda wa ajali hiyo Peter Zebedayo ambaye ni manusura anasema wakati wa kuogelea wenzake walizama na walipojaribu kuibuka walishindwa ambapo  jitihada za kuwaokoa zilikwama.

Shuhuda mwingine Debora Mgundwa, amesema katika eneo hilo ijumaa ya wiki iliyopita mtu mwingine alifariki katika eneo hilo.  

Mfinanga amewataka wananchi kuchukua tahadhari wanapokuwa kwenye eneo hilo kutalii ili kuepuka maafa kama hayo haswa katika kipindi hiki ambacho maji yanaongezeka kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...