Monday, January 11, 2021

Lukuvi Ataka Usimamizi Wa Ardhi Katika Ngazi Ya Mitaa


Na Munir Shemweta, WANMM SINGIDA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuhakikisha zinashusha usimamizi wa masuala ya ardhi katika ngazi za mitaa na vijiji ili ziweze  kusimamia kuepuka ujenzi holela na kurahisisha ufuatiliaji makusanyo ya kodi ya pango la ardhi.

Akizungumza wakati akikagua ofisi ya ardhi katika halmashauri ya Manispaa ya Singida akiwa katika ziara ya siku moja kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Singida tarehe 10 Januari 2021, Lukuvi alisema ni vyema wakurugenzi katika halmashauri nchini kuwapa wajibu watendaji wa mitaa na vijiji kwa barua kusimamia misingi ya ardhi yenye lengo la kusimimia sheria katika masuala ya ardhi.

Hata hivyo, Waziri Lukuvi alisema Watendaji wa Mitaa na Vijiji watakaokasimia mamlaka ya usimamizi ardhi katika maeneo yao hawatakuwa na jukumu la kugawa, kupanga, kupima na kumilikisha ardhi bali kuangalia yanayoendelea katika mitaa yao na wakikuta ukiukwaji wowote kama vile ujenzi holela basi watakuwa na wajibu wa kusitisha.

" Afisa ardhi katika wilaya hawezi kujua yale yanayoendelea kwenye mtaa au kijiji na hata suala la kodi  mkiwatumia watendaji wa mitaa wataweza kusaidia kuwabaini wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi kirahisi"

Ametaka watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri kuhakikisha wanatengeneza majedwali maalum yenye orodha inayoonesha kila mmiliki wa kiwanja kwa lengo la kuwawezesha watendaji wa mitaa kuwajua wamiliki katika maeneo yao.

" Kumbukumbu zote za masuala ya ardhi wajulishwe watendaji wa mitaa na vijiji ili waweze kufuatilia katika mitaa yao maana katika suala la hati za kimila tumefanya vizur ngazi ya vijiji ila suala la Hati Miliki za Ardhi bado tuko nyuma maana tumeficha taarifa wilayani" alisema Lukuvi.

Waziri Lukuvi alizitaka ofisi za ardhi za mikoa kuhakikisha zitatoa elimu kwa watendaji wa mitaa na vijiji ili kuwajengea ufahamu wa masuala ya ardhi na kuwawezesha kusimamia vyema masuala hayo katika maeneo yao.

Kwa mujibu wa Lukuvi, hata kama Manispaa imepanga matumizi bora ya ardhi ni vyema matumizi yake yakawekwa kwenye vipande vya ngazi ya mitaa na kusisitiza kuwa kazi hiyo ni ya halmashauri kwa kuwa mitaa ni jicho lake la kutoa taarifa katika masuala mbalimbali yakiwemo yale ya ardhi.

Katika ziara yake Waziri wa Ardhi mbali na kutembelea halmashauri za wilaya ya Singida na Ikungi na kusisitiza kuwa halmashauri ndizo zenye jukumu la kupanga, kupima na kumilikisha ardhi katika maeneo yake na jukumu hilo siyo la maafisa ardhi.

Lukuvi alisema Halmashauri zote zijue zina wajibu wa kusimamia ardhi katika maeneo yao na ilichofanya Wizara ya Ardhi ni kuwapatia wataalam watakaowasaidia kujua namna bora  ya kutumia ardhi vizuri.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...