Sunday, January 10, 2021

GARI LA KAMANDA WA POLISI GEITA, HIACE ZATEKETEA MOTO, CHANZO BODA MWENYE DIZELI


Na Rehema Matowo - Mwananchi
Gari ya Kamanda wa polisi mkoa wa Geita na gari ndogo ya abiria aina ya Hiace leo mchana zimewaka moto na kuteketea baada ya ajali iliyosababishwa na dereva boda boda aliyekuwa amebeba mafuta ya dizeli.

Hata hivyo, Kamanda wa polisi mkoa wa Geita, Hendry Mwaibambe hakuwemo kwenye gari hiyo na amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema imetokea leo majira ya saa 8.46 mchana katika eneo la Makurugusi wilayani Chato mkoani Geita.

Katika ajali hiyo, dereva wa boda boda ambaye inasemekana amepoteza maisha huku watu 16 wakijeruhiwa ambapo wawili kati yao ni askari polisi.

Akielezea tukio hilo, Kamanda Mwaibambe amesema dereva wa boda boda huyo alikuwa amebeba lita 100 za mafuta ya dizeli akaingia barabarani bila umakini na kugongwa na gari ya kamanda kisha kwenda kugonga hiace iliyokuwa imeegeshwa pembezoni mwa barabara na kusababisha magari yote kuwaka moto .

Amesema gari hiyo ya polisi yenye namba PT 4447 iliyokuwa ikiendeshwa na Koplo Manase Nestory imewaka moto kufuatia cheche za pikipiki baada ya ajali kuangukia mafuta yaliyomwagika.

Kwa mujibu wa kamanda, majeruhi wamekimbizwa hospitali ya wilaya ya Chato na kwamba hali ya dereva wa Hiace ni mbaya huku polisi wakitibiwa na kuruhusiwa kuondoka.



Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...