Friday, December 25, 2020

Polisi walivyomteka mfanyabiashara, kuomba Sh30 mil

 



Watu tisa wakiwamo askari polisi watatu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumteka mwenyekiti wa Chama cha Wauza Madini Tanzania (Tamida), Sammy Mollel na kumwomba rushwa ya Sh30 milioni.


Watuhumiwa wanadaiwa kumteka Mollel anayemiliki kampuni ya Germs and Rock Ventures wakijitambulisha wametoka makao makuu ya jeshi hilo kikosi maalum kinachofuatilia ukwepaji kodi.


Kamanda wa polisi Arusha, Salum Hamduni amesema tukio hilo limetokea Desemba 14 likiwahusisha askari namba H125 Gasper Paul wa kitengo cha intelijensia makao makuu Dodoma, G5134 DC Heavenlight Mushi wa kitengo cha intelijensia Kinondoni na H1021 PC Bryton Murumbe wa Dodoma.


Wengine waliokamatwa ni Lucas Mdeme, meneja wa kampuni ya Crown Lapidary ya jijini Arusha, Shabani Benson (49) mfanyabiashara jijini Dodoma na Nelson Lyimo (58) mfanyabiashara wa Kimandolu Arusha. Kwenye orodha hiyo pia kuna Leonia Joseph (40), katibu muhtasi wa kampuni ya Germs & Rocks Ventures, Omary Mario (43) mfanyaviashara eneo la Olorieni Arusha na Joseph Chacha (43) mfanyabiashara wa Elboru Arusha.


"Awali polisi iliwakamata DC Muchi, PC Murumbe na mfanyabiashara Benson baada ya kushawishi na kupokea rushwa na baadaye watuhumiwa wengine sita," alisema Hamduni.


Taarifa za awali zinasema watuhumiwa waliomba Sh30 milioni na walipokea Sh10 milioni lakini walikamatwa walipofuata kiasi kilichobaki.


Baadhi ya walioshuhudia kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo, walisema mchana wa Desemba 12 watuhumiwa walienda Germs & Rock Ventures na kumchukua Mollel wakidai anakwepa kodi.


Mollel mwenyewe alisema wakiwa njiani baada ya kukamatwa na watuhumiwa hao waliokuwa na silaha walimuomba fedha.


"Kwa sasa siwezi kufafanua zaidi, uchunguzi bado unaendelea," alisema Mollel.


Shuhuda wa tukio hilo kwa sharti la jina lake kutotajwa gazetini alisema alikuwa ofisini kwa mfanyabiashara huyo wakati polisi hao wanafika na walijitambulisha kuwa wanatokea makao makuu.


Alisema walifika ofisini hapo watu wanne, watatu waliingia ndani ya ofisi na mmoja alibaki nje na baada ya muda walitoka na Mollel akiwa chini ya ulinzi.


"Mimi nilikuwa hapa kwenye viti walikuja na kutokuta hapa kisha, kumtoa Mollel akiwa chini ya ulinzi na walinyang'anya silaha yake na kuondoka naye kutumia gari dogo ambalo linashikiliwa na polisi,"alisema.


Shuhuda mwingine alisema watuhumiwa hao walimuachia Mollel maeneo ya Makuyuni baada ya kukubaliana kuwa atoe Sh30 milioni na kwa kuwa alikuwa hana aliagiza Arusha kupelekewa Sh10 milioni na nyingine angetoa siku ya Jumatatu Desemba 14.


Alibainisha kuwa Mollel alipoachiwa alianza kuwafuatilia watu hao na kubaini kuwa hawakutumwa kama walivyodai, "Mollel alitoa taarifa kwa vyombo vya usalama na kufanikiwa kuwakamata hiyo Jumatatu walipokwenda kuchukua Sh20 milioni zilizobaki."

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...