Friday, December 25, 2020

Mondi Awateka Mastaa Marekani




MUZIKI wa Bongo Fleva sasa unakwenda kwa mwendo wa mateka, mikono juu duniani kote; acha ubishi wako.  Msanii Nasibu Abdul 'Diamond' au Mondi amefanikiwa kuwateka baadhi ya wasanii mastaa wa Marekani kiasi cha kumvulia kofia.

 

Alipoanza kukiwasha kimuziki Mondi alifanikiwa kufanya kolabo matata za mapema na mastaa wa Marekani kama Neyo (Marry You), Rick Ross (Waka) ambao ulifungiwa na serikali kwa kukosa maadili) na Omario (African Beauty).

Hatua hiyo ilileta mapinduzi ya kifikra miongoni wa Wabongo na hivyo kuanza kuamini kuwa, gari la muziki wao limewaka na ndoto za kufika mbali ziliwatokea wengi.

 

BALAA LA MONDI

Akiwa kama msanii anayesema "hakuna kulala hadi kieleweke" Mondi hakutaka kupangua gia ya ustadi wake kimuziki ambapo mwaka huu alifanikiwa kumshika mwanadada staa wa Marekani, Alicia Keys.

Tofauti na mazoea ya wasanii wa Kibongo kujibembembeza kwa wasanii wa ng'ambo safari hii ilikuwa zamu ya Alicia Keys kumuomba kolabo Mondi ambapo alifanya naye ngoma iitwayo Wasted Energy.

 

Wakati kishindo cha ngoma hiyo kikiwa bado hakijaisha, Mondi ameendelea kuwa lulu kwa wasanii wa marekani ambapo hivi karibuni rapa maarufu P Diddy alimkubali msanii huyo wa Bongo kwa kum-follow kwenye ukurasa wake wa Intagram jambo ambalo lilileta mshangao kwa wengi.

 

Mwishoni mwa wiki iliyopita staa mwingine wa Marekani, Janet Jackson, mtoto wa nguli wa muziki duniani Michael Jackson, aliposti video ya ngoma mpya ya Mondi iitwayo Waah.

Hivi sasa Waah ambayo ndiyo mfalme mjini YouTube kwa kufikisha takriban watazamaji milioni 19, utamu wake ulimwingia Janet na kujikuta akiupaisha kwenye ukurasa wake wa Instagram uliofuatiliwa na watu milioni tano na ushee.

 

Licha ya mwanamuziki huyo wa kike wa Marekani kuchukua video hiyo kupitia kwenye ukurasa wa Masaka Kids, watoto wanaocheza miziki mbalimbali mitandaoni kutoka nchini Uganda, Mondi alipoona kitendo hicho alikenua meno na kuandika kwenye ukurasa wake wa Instagram:

 

"WAAH love from the icon @ janetjackson… This means a lot to me."

Akimaanisa; Waah kupendwa na staa Janet Jackson jambo hilo lina maana kubwa kwake.

Meneja wa Mondi, Said Fella naye hakujitenga na furaha hiyo alijitokeza kwenye ukurasa wa Janet na kushukuru huku akiwaambia waandishi wetu waliompigia simu kumuuliza kuhusu kitendo hicho cha msanii wa Marekani, kuwa anajisikia mwenye furaha.

 

2020 MWAKA MTAMU KWA MONDI

Licha ya kuwepo kwa changamoto za ugonjwa wa Corona ambao umeathiri pakubwa sanaa na harakati nyingi za kimaisha duniani mwaka 2020, Mondi amekuwa kwenye mafanikio makubwa ndani ya mwaka huu wenye changamoto.

 

Mbali na Mondi kama bosi wa Lebo ya Wasafi Classic Baby 'WCB' wasanii waliopo chini yake kama Zuhura Othman 'Zuchu', Mbwana Kilungi 'Mbosso' na Raymond Shaban 'Rayvanny' nao wamefanya vizuri kimuziki kwenye mwaka huu ambao unaelekea ukingoni.

 

Ukiweka kando wimbo wa Waah aliomshirikisha mwanamuziki nguli kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Koffi Olomide kuweka rekodi ya ajabu kwa kutazamwa na watu wengi kwa muda mfupi mwishoni mwa wiki iliyopita Mondi alitunukiwa tuzo ya Msanii Bora wa Kiume wa Mwaka kwenye tuzo zinazotolewa na na waandaji AEAUSA wa nchini Marekani.

 

Msanii mwingine kutoka Lebo ya WCB aliyechukua tuzo hizo ni 'Rayvanny' ambaye amechukua tuzo ya Msanii Bora wa Kiume ukanda wa Mashariki, Kusini na Kaskazini mwa Afrika.

Msanii mwingine wa Bongo aliyetwaa tuzo hizo za AEAUSA ni Faustina Charles Mfinanga 'Nandy' ambaye alitwaa tuzo ya Msanii Bora wa Kike wa Mwaka.

 

AMA KWELI GARI LIMEWAKA

Kufuatia mafanikio ya muziki wa Bongo kuendelea kupenya kimataifa na kitendo cha Mondi kuwashika mastaa wakubwa nchini Marekani wadau wa muziki hasa kwenye mitandao ya kijamii wamesema ni kama gari la sanaa za Bongo limewaka.

 

"Kwa miaka mingi tumekuwa watumwa wa muziki wa Kimarekani, lakini hiki kinachondelea hivi sasa jamaa wameshasalimu amri kikubwa ni wasanii wetu wazidishe bidii hadi tutwae ufalme," aliandika mtu mmoja kwenye mtandao wa kijamii ambao ulikuwa unajadili mafanikio ya Mondi na muziki wa Bongo kwa ujumla wake.

 

Mjadala ulikuwa mpana kwenye mitandao ya kijamii kiasi cha watu kukumbusha jinsi wasanii wa Marekani miaka ya nyuma walivyokuwa na 'nyodo' ya kuja Bongo kufanya shoo.

"Marehemu Ruge (Mutahaba) kahangaika kweli na hawa wasanii wa Marekani kumleta mtu kama Rick Ross haikuwa shughuli ya kitoto na walikuwa wakifika wanakuwa kama malaika fulani hivi kwa Wabongo," aliandika mtu mwingine.

 

SERIKALI YAJIPANGA KUWAINUA WASANII

Hivi karibuni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hassan Abbas amesema serikali imepania kuwainua wasanii kwa kuwashika mkono katika kazi zao sambamba na kuweka utaratibu wa uwepo wa mfuko wa wasanii kwa ajili ya kuwaendeleza.

 

Mipango hiyo ya serikali imepokewa kwa mikono mwili na wasanii ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakilalama kunyonywa jasho lao kiasi cha kutonufaika na kazi zao.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...