Mashirika ya kutoa msaada yanasema dawa za kupunguza makali ya virusi vya ukimwi zenye ladha tamu ya matunda ya 'strawberry' kwa ajili ya watoto zitaanza kutolewa katika nchi za Afrika kuanzia mwakani.
Hizo zitakuwa ni dawa za kwanza zenye ladha tamu kukabiliana na VVU kupatikana kwa ajili ya watoto.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watoto milioni 1.5 kote duniani wanaishi na virusi vya ukimwi lakini wanasema ni nusu tu ya idadi hiyo ndio wanaopokea matibabu.
Moja ya kile inachofanya hali kuwa ngumu kwa watoto wadogo kunywa dawa za virusi vya ukimwi ni ladha yake chungu.
Wataalamu wa Afya wanasema sasa hatua ya kusaidia kukabiliana na hali hiyo inawadia – dawa zenye ladha tamu zitakuwa muafaka kabisa kwa watoto wenye VVU.
Na pia hatua hiyo inamaanisha hakutakuwa na haja ya kuvunja mara mbili dawa za watu wazima kwa ajili ya watoto.
Tatizo jingine limekuwa gharamu ya juu – licha ya hatua kubwa kupigwa miaka ya hivi karibuni.
Katika kipindi cha miaka michache ijayo, nchi za Benin, Kenya, Malawi, Nigeria na Zimbabwe zitaanza kupokea dawa hizo mpya.
Lakini pia gharama yake itakuwa ya chini kwasababu badala ya kutumia karibu dola 500 sawa na (£372) kwa mwaka, dawa hizo mpya zitagharimu dola 120.