Na Omary Mngindo, Chalinze
HALMASHAURI ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani katika bajeti yake ya mwaka wa fedha wa 2020/2021 inakadiria kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 39.7.
Hayo yamo katika taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Ramadhani Possi, aliyoisoma mbele ya Madiwani hao muda mfupi baada ya kuapishwa, tayari kuanza majukumu ya kuwatumikia wananchi.
Katika hafla hiyo iliyokuwa mbele ya Katibu Tawala Kasilda Mgeni aliyekuwa Mwenyekiti wa muda, pia alikuwepo Katibu wa CCM Gertrude Sinyinza, Katibu Mwenezi John Fransis, Aeshi Rajabu Katibu wa Jumuia ya Wazazi wilaya na Kamatinya Ulinzi na Usalama ya wilaya.
Imeeleza kuwa katika makadirio hayo vyanzo vya ndani sh. bilioni 10.9, ruzuku kutoka Serikali Kuu pamoja na wahisani sh. bilioni 28.8 huku michango kutoka kwa wananchi sh. milioni 984, ambapo mpaka Nov 30 mwaka huu sh. bilioni 3.4 zimekusanywa kutoka vyanzo vyake sawa na asilimia 38.
"Makisio ya halmashauri ya Chalinze kwa mwaka wa fedha wa 2020/2021 inakadirwa kutumia sh. bilioni 39.7 kwa ajili ya matumizi ya kawaida (OC), mishahara (PE) na miradi ya maendeleo pamoja na nguvu za wananchi," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Imeongeza kuwa makadirio hayo mishahara sh. bilioni 18.6 (ruzuku), matumizi mengineyo (OC) bilioni 1.6, miradi ya maendeleo (ruzuku), bilioni 8.4 (ruzuku) huku matumizi mengineyo na miradi ya maendeleo bilioni 10.9, matumizi ya michango ya wananchi inakadiriwa sh. bilioni 984.
Aidha imepongeza kitengo cha TEHAMA, Habari, na mahusiano ambacho kwa kipindi cha Julai mpaka Novemba kimetekeleza mambo mbalimbali ikiwemo utoaji wa taarifa ya mambo mbalimbali yaliyofanyika.
"Halmashauri kupitia kitengo cha habari imetangaza kazi kwa njia ya tovuti na mitandao ya kijamii, kutoka msaada wa kiufundi kwa mfumo wa GOTHIMIS na FFARS, kusimamia uanzishaji wa mfumo mipya ya TEHAMA na kutatua changamoto kwenye machine za kieletroniki ," ilieleza.
Pia katika kuhakikisha kuwa habari za kimaendeleo zinawafikia wananchi, halmashauri kupitia kitengo cha habari kimekuwa kikishirikiana na vyombo vya habari kama vile Televisheni, magazeti, radio na blog ambapo wananchi wametambua kazi zinazotekelezwa.