MGOMBEA wa urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ametangaza kutokubali matokeo ya uchaguzi yanayoendelea kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kufuatia uchaguzi mkuu uliyofanyika jana Oktoba 28, 2020 nchi nzima.
Amedai kuwa kuwa uchaguzi huo ulianza kuingia dosari mapema katika kuapisha mawakala ambao ndiyo waangalizi wa uchaguzi kwa niaba ya chama chao.
Aidha amewataka Watanzania kudai haki yao kwa njia ya demokrasia na siyo kwa vurugu yoyote huku akisema jumuiya za kimataifa pamoja na jumuiya za kikanda ziingilie kati taarifa za matokeo ya uchaguzi wa Tanzania.
"EAC, SADC wasitoe taarifa za kuhalalisha uchaguzi huu. Waseme ukweli. Watanzania waingilie kudai haki yao kwa amani kwa njia ya kidemokrasia," amesema Lissu katika mkutano na waandishi wa habari.
Lissu ameongeza kusema kuwa chama chake kimeweka wagombea 244 wa ubunge nchi nzima, kati ya hao 63 walienguliwa, udiwani 3,754 kati yao wagombea 1,025 walienguliwa, hivyo takribani 30% walienguliwa- 'haijawahi kutokea tangu tumefanya uchaguzi wa vyama vingi nchini".
Aliongeza kusema kuwa mbali na kuwa kulikua na changamoto ya kutokuwa na fedha, hawakuweka picha za mgombea nchi nzima lakini "Watanzania walituunga mkono". Jana Lissu alisifu zoezi la upigaji kura kuwa limekwenda vizuri baada ya kumaliza kupiga kura katika jimbo lake la Singida Mashariki.
Hata hivyo Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeshakanusha madai hayo ya upinzani na kusema tuhuma zinazotolewa hazijawasilishwa rasmi na sasa inaendelea na zoezi la kupokea matokeo kutoka katika majimbo mbalimbali na kuyatangaza kwa wananchi kupitia vyombo vya habari.