Wananchi wa Afrika Kusini wanaopinga kutolewa chanjo ya corona jana waliandamana katika mji wa Johannesburg wakieleza kusikitishwa kwao na majaribio ya kwanza ya chanjo hiyo kufanywa kwa binadamu barani Afrika kwa ajili ya chanjo ya corona.
Jumatano iliyopita, wataalamu wa Chuo Kikuu cha Witwatersrand cha nchini Afrika Kusini kwa ushirikiano na kile cha Oxford waliandaa chanjo ya kwanza ya majaribio kuwahi kufanywa nchini Afrika Kusini ambayo itawahusisha watu waliojitolea 2000.
Taarifa zinasema kuwa, kujumuishwa nchi ya Afrika Kusini katika majaribio ya chanjo hiyo ya corona kumesudiwa ili kuhakikisha kuwa, bara la Afrika linapata chanjo hiyo kwa gharama nafuu na lisiachwe nyuma katika uwanja huo.
Waandamanaji walikusanyika mbele ya Chuo Kikuu cha Witwatersrand katika mji wa Johannesburg wakipiga nara za "hatutaki Waafrika kutumiwa kama nguruwe wa Guinea." Waandamanaji hao wamehoji kwamba inakuwa vipi watu wafanyiwe majaribio ya chanjo hiyo ya corona bila ya kujua hatari na madhara yake? Wamesema majaribio hayo yaliyopangwa kufanywa nchini Afrika Kusini kwanza yanapasa kufanyiwa kwa watoto wa wabunge na wa mawaziri na si kwa watu maskini wa nchi hiyo.
Afrika Kusini ina idadi kubwa ya watu walioambukizwa virusi vya corona barani Afrika ambapo hadi sasa nchi hiyo imethibitisha kesi zaidi ya 150,000 na vifo zaidi ya 2,600.
Source