Sunday, June 21, 2020

Serikali Yamchunguza Zari! Kisa Kuwatusi Watanzania



Siku kadhaa baada ya mwanamama mjasiriamali na mzazi mwenza wa staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul 'Diamond Platnumz', Zarinah Hassan 'Zari The Boss Lady' kuwatusi Watanzania, hatimaye Serikali imesema inachunguza jambo hilo.



Gazeti la IJUMAA limezungumza na viongozi mbalimbali ambao baadhi yao wamesema taratibu zikifanyika, huwenda mwanamama huyo akachukuliwa hatua za kinidhamu."Samahani, mmezaa vitoto vyenye havina akili, havina confidence (havijiamini), haviwezi kuongea, yaani vimekuwa kama vindondocha…"



Hiyo ni sehemu ya maneno kwenye hotuba ya Zari ya takriban saa moja ya kuwachamba Watanzania wanaomfuatilia maisha yake.


Kauli hizo na nyingine nyingi zenye lengo la kuwatusi Watanzania, zilisababisha baadhi ya watu kuja juu kwa kudai amewatukania watoto wao.



"Sisi kama Watanzania, tunatoa malalamiko yetu kama wananchi, haijalishi tupo nchini au hatupo, hivi Serikali inaona hii dharau aliyoifanya mwanamke wa Diamond?



"Kuidhalilisha nchi yetu, kudhalilisha watoto wetu, hata kama alikuwa anatukanwa na baadhi ya watu, lakini siyo Watanzania wote waliomtukana hadi kuita watoto wetu mandondocha.



"Ina maana ni watoto wetu wote, alafu anaiita Tanzania ni shimo la umaskini, kwa nini Serikali isimpe onyo kwa kutokanyaga Tanzania mpaka atakapojirekebisha na kutuomba msamaha Watanzania wote?



"Haiwezekani aidharau nchi yetu, halafu aendelee kuja na kufanya kazi kwenye nchi aliyoiita ina watu mandondocha," aliandika @anifalahmad katika ukurasa wake wa Mtandao wa Instagram.Kufuatia malalamiko na kelele nyingi kuwa, Zari amewakosea heshima Wabongo, Gazeti la IJUMAA lilifanya jitihada za kumfikia Kaimu Meneja wa Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Semu Mwakanjala ambaye yeye kwa upande wake, alisema kuwa hana mamlaka ya kuzungumzia suala hilo.



Alisema kuwa, wapo watu husika ambao wao ndiyo wanaweza kutoa tamko juu ya hilo."Hilo alilolifanya ni kama kosa la jinai, hivyo binafsi siwezi kutoa kauli yoyote kwa sababu kuna watu ambao ndiyo wahusika wa kuweza kuzungumzia hilo, hivyo watafute na ukishawapata, na wao wakafanya uchunguzi na kubaini tatizo, basi watasema ni hatua gani ambazo watazichukua," alisema Semu.



Hata hivyo, IJUMAA halikuishia hapo, kwani liliwafikia Idara ya Polisi ya Makosa ya Mtandaoni (cyber crime) na kuzungumza na Polisi aliyejitambulisha kwa jina moja la Mwangasa ambaye naye kwa upande wake alikuwa na haya ya kusema;"Mimi naona cha kufanya labda nikushauri kwa sababu huyu Zari amewahi kuwa msanii, hivyo ungewatafuta watu wa Idara ya Habari na wao pia wana sehemu yao, wanaweza kuzungumza kwa sababu kwa suala la jinai, nikiangalia sana, inawezekana, lakini ni suala la kinidhamu ambalo hata watu wa habari wanaweza kuzungumza wanalichukuliaje hilo.



Ingawa pia mtu ambaye anaona ameongelewa vibaya, anaweza kwenda kulalamika Polisi."Kutoka hapo, IJUMAA lilimtafuta pia Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, Kamanda David Misime ambaye naye kwa upande wake alihitaji kuiona video hiyo kisha ndipo atoe tamko lake.



"Nadhani mpaka niione hiyo video kisha ndiyo nitatoa tamko langu," alisema kamanda huyo na kutumia video hiyo kwa ajili ya uchunguzi ambapo gazeti hili linafuatilia kitakachojiri.

Stori:MEMORISE RICHARD, Ijumaa
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...