Sunday, June 21, 2020

Majaliwa atangaza dawa kwa wachochezi


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imewaagiza Makamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) nchini kuwakamata na kuwachukulia hatua watu wote watakaojihusisha na vitendo vya rushwa kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Ametoa kauli hiyo Jumamosi, Juni 20, 2020 wakati akizungumza na viongozi wa mkoa wa Lindi mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Nachingwea akiwa njiani kuelekea wilayani Ruangwa kwa ziara ya kikazi.

"Watu wamezoea vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi, Serikali tumeagiza kwa kamati za ulinzi na usalama zishirikiane kuhakikisha kwamba hakuna vitendo vya rushwa katika uchaguzi na yeyote ambaye anajihusisha na rushwa asiachwe", amesema.

Vilevile, Waziri Mkuu amewataka Makamanda wa TAKUKURU katika wilaya zote nchini wahakikishe wanawakamata watu wote watakaojihusisha na vitendo vya rushwa wakiwemo na wapambe ambao ndio wachochezi wa vitendo hivyo.

Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo ili kuhakikisha Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu unakuwa huru na wa haki, hivyo kuwawezesha wananchi kuchagua viongozi wanaowahitaji na si kwa msukumo wa rushwa.

Katika hotuba yake aliyoisoma Juni 15, 2020 bungeni jijini Dodoma wakati akihitimisha mkutano wa 19 wa Bunge, Waziri Mkuu aliwataka viongozi wa vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi wazingatie katiba, sheria, kanuni na miongozo iliyopo katika uendeshaji wa shughuli za uchaguzi.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwasihi viongozi na wanachama wa vyama vyote vya siasa na wananchi kwa ujumla waendelee kulinda amani na kuendeleza mshikamano katika kipindi hiki na wakati wa Uchaguzi Mkuu.


Source
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...