NGUMI ni miongoni mwa michezo ambayo imeitangaza na kuipa heshima Tanzania duniani kutokana na mabondia wake kuonyesha uwezo mkubwa na kushinda katika mapambano mbalimbali ya Kimataifa.
Kutokana na sababu mbalimbali za kiutendaji wa viongozi wa mchezo huu, ulipoteza sifa yake Kitaifa na Kimataifa na kudidimiza maendeleo yake hapa nchini. Eleuteri Mangi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dodoma anaelezea jinsi mchezo huo unavyorejesha heshima iliyokuwa nayo Tanzania Kitaifa na Kimataifa katika miaka ya 1970.
Kutokana na sababu mbalimbali za kiutendaji wa viongozi wa mchezo huu, ulipoteza sifa yake Kitaifa na Kimataifa na kudidimiza maendeleo yake hapa nchini. Eleuteri Mangi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dodoma anaelezea jinsi mchezo huo unavyorejesha heshima iliyokuwa nayo Tanzania Kitaifa na Kimataifa katika miaka ya 1970.
Mchezo wa ngumi ni miongoni mwa michezo inayofahamika na kupendwa sana na watu wengi duniani. Kama ilivyo kwa michezo mingine kama vile mpira wa miguu, mchezo huu umekuwa ni chanzo cha ajira na hivyo kujipatia umaarufu mkubwa ambapo vijana wengi wanajiunga kwa lengo la kujipatia kipato. Ndiyo kusema, michezo ni kiwanda kikubwa kinachobeba ajira lukuki kwa vijana na wataalam wa michezo mbalimbali nchini na duniani kote.
Mchezo wa ngumi nchini Tanzania ulianza kufahamika katika miaka ya 1950 ambapo miaka ya 1970 mabondia wake walianza kufahamika katika mashindando mbalimbali ya Kimataifa. Medali ya kwanza ya Kimataifa ililetwa na Titus Simba mwaka 1974 katika michezo ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika nchini Uingereza na mwaka 1998 bondia mwingine Michael Yombayomba aliiletea Tanzania medali nyingine katika mashindano hayo ya Jumuiya ya Madola yaliyofanyika nchini Malasia.
Huo ndio ulikuwa mwanzo wa Tanzania kufahamika Kimataifa katika medani ya mchezo wa ngumi ambapo wanamasumbwi wengine kama vile akina Makoye Isangula, Stanrey Mabesi, Benjamin Mwangata, Shaaban Matumla na wengine walitamba na kuiletea Tanzania medali mbalimbali. Hata hivyo, kuzuka kwa vyama vingi vya ngumi nchini kumekuwa chanzo cha kushuka kwa mchezo huo katika kipindi cha muongo mmoja uliopita kutokana na viongozi wake kutoelewana kiutendaji kutokana na sababu mbalimbali.
Kwa kulitambua hili, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Johh Pombe Magufuli kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imeanza kuchukua hatua kadhaa kuweza kurejesha heshima ya Tanzania Kitaifa na Kimataifa kupitia mchezo wa ngumi.
Kuundwa kwa Kamisheni ya Kusimamia Ngumi za Kulipwa nchini (TPBRC) ni mwanzo mpya unaodhihirisha nia ya dhati ya Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe (Mb). Utekelezaji wa agizo la kuanzisha TPBRC nchini umeanza kuleta manufaa kutokana na shabaha ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020 katika kukuza michezo.
Ilani hiyo katika ukurasa wake wa 218 Ibara ya 161 imetamka "Katika kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015-2020 imebainisha CCM itaielekeza Serikali kuimarisha sekta ya michezo ili kuinua kiwango cha michezo nchini ikiwa ni pamoja kuifanya sekta ya michezo kutoa fursa za ajira hususani kwa vijana".
Kama michezo mingine, mchezo wa ngumi za kulipwa unaendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa Na. 12 ya mwaka 1967 na marekebisho yake Na. 6 ya mwaka 1971 pamoja na kanuni za Usajili Na. 442 za mwaka1999.
Sheria hiyo iliyofanyiwa marekebisho ya Sheria Na. 3 kifungu cha 18 ya mwaka 2018 kwa mamlaka aliyonayo Waziri mwenye dhamana ya michezo nchini yameongeza wigo na kutambua michezo ya ridhaa na michezo mingine ambayo yamepelekea kuundwa kwa Kamisheni ya Ngumi za kulipwa nchini.
Chombo hicho kimeleta mafanikio katika mchezo wa ngumi za kulipwa nchini na umekuwa na mchango mkubwa katika kuajiri vijana ambao wamekuwa na mafanikio kwa mtu mmoja mmoja akiwa mchezaji na taifa kwa ujumla.
Katika kuthamini michezo nchini ikiwemo masumbwi, Rais Dkt. Magufuli ni mpenda michezo amekuwa mstari wa mbele katika kutambua na kuwatuza wanamichezo wanapofanya vizuri katika mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Mapema mwezi Machi mwaka 2019, Rais alidhihirisha uzalendo wake kwa michezo nchini kwa kuwapa wachezaji, viongozi wao na bondia Hassan Mwakinyo zawadi ya viwanja vya kujengea nyumba mkoani Dodoma kama ishara ya kuonyesha alivyofurahishwa kwa juhudi za wachezaji na viongozi wao kuipa Tanzania ushindi.
"Nimeamua niwape zawadi kidogo kwa niaba ya watanzania, nitawapatia viwanja vya kujenga nyumba wachezaji wote wa Taifa Stars na viongozi wao, bondia Hassan Mwakinyo pamoja na mwalimu wako, zawadi hiyo pia kwa Peter Tino na Leodegar Tenga" alisema Rais Dkt. Magufuli.
Bondia Hassan Mwakinyo anapongezwa kwa kazi nzuri anayoendelea kuliwakilisha taifa vema katika mashindano mbalimbali duniani ikiwemo kumtwanga Amel Tinampay raia wa Ufilipino kwa point katika mchezo uliofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Novemba, 2019.
Hakika mchezo wa ngumi za kulipwa umekuwa mwanzo mpya wa mabondia nchini kufanya vizuri katika mapambano waliyoshiriki. Bondia Abdallah Paziwapazi alimchapa Zulipikaer Maimaitiali raia wa China kwa Knock Out katika pambano la WBO Asia Pacific Super Middle Title lililofanyika nchini China mwezi Agosti, 2019 wakati Hamis Maya alimtwanga Piergiulia Ruhe raia wa Ujerumani kwa Knock Out katika pambano la Global Boxing Council Intercontinental Welter lililofanyika nchini Ujerumani mwezi Novemba, 2019.
Mabondia wengine waliofanya vizuri na kuliletea Taifa sifa nzuri ni pamoja na Bondia Bruno Melkiory Tarimo (Vifua Viwili) ambaye alimpiga Nathaniel May raia wa Australia kwa point katika pambano la Boxing Federation International Super Feather Title lililofanyika nchini Australia mwezi Desemba, 2019 na Bondia Salimu Jengo aliyemchapa Suriya Tatakhun raia wa Thailand kwa KO katika pambano la Universal Boxing Organization World Light Title lililofanyika Jijini Tanga mwezi Januari, 2020.
Akiwasilisha Bajeti ya Wizara yake ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka 2020/2021 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amewapongeza wachezaji wa Kitanzania wanaozidi kuongezeka na kufuzu vigezo vya kimataifa na kucheza michezo ya kulipwa katika nchi mbalimbali na kupeperusha vyema bendera ya Tanzania.
"Nawapongeza wanamichezo wote nchini kwa kupeperusha vyema bendera ya nchi yetu katika mashindano mbalimbali ya kimataifa na hivyo kuitangaza na kuiletea heshima kubwa nchi yetu" alisema Dkt. Mwakyembe.
Waziri Mwakyembe aliendelea kusema "Namshukuru sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake thabiti na hatua anazochukua kuimarisha michezo nchini. Nampongeza Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kwa kuipa wizara yangu ushirikiano mkubwa na msaada katika kuendeleza michezo nchini. Pia niwapongeze watanzania kwa hamasa na uzalendo wanaouonesha kwa timu zetu".
Kwa upande wake Promota Shomari Kimbau ambaye ni mdau wa mchezo wa masumbwi ameipongeza Serikali kwa kwa nia yake ya dhati ya kusaidia na kusimamia mchezo huo na kuamini usimamizi bora wa mchezo huo nchini ni mwanzo mpya wa Mchezo wa Ngumi za Kulipwa.
"Lazima yawepo mazingira mazuri ya kusimamia mchezo huu, ili upendwe na watu wengine pamoja na kurudisha imani kwa wadau na wawekezaji waweze kuwekeza fedha zao. Hiki kinachofanywa na Serikali ni kitu kizuri na kinafaa kuungwa mkono na wadau wa mchezo huu" anasema Kimbau.
Awali Ngumi za Kulipwa zilisimamiwa na Vyama tofauti tofauti ikiwemo Chama cha Wataalamu wa Mchezo wa Ngumi Tanzania (TPBO), Pugilistic organization of Tanzania (PST) na Tume ya Wataalamu wa Mchezo wa Ngumi Tanzania (TPBC).
Mtindo huo wa kuongoza mchezo wa ngumi za kulipwa ulikuwa na namna ya vionozi na wachezaji kutoelewana wenyewe kwa wenyewe kabla ya Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuingilia kati mgogoro huo na kuamua kufanya mabadiliko katika mchezo wa Ngumi za Kulipwa ndipo TPBRC ilipoanzishwa na kupewa mamlaka ya kusimamia Ngumi za Kulipwa mnamo mwaka 2018.
Kwa mujibu wa BMT, baada ya kuundwa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa yapo mafanikio yanayodhihirisha kuimarika kwa mchezo huo yanayochagizwa kuwepo kwa viongozi waliopatikana kwa uchaguzi uliofanyika Machi 31, 2019 ambao ni Joe Anea (Rais), Agapita Basil Jambwale (Makamu wa Rais), Yahya Poli (Katibu Mkuu), Bakari Songoro (Mweka Hazina), Hamisi Kimanga na Nassoro Chuma (Wajumbe).
Aidha, kuunganishwa kwa wadau wa ngumi za kulipwa umeibua mwamko mpya kwa wadau hao, mabondia wanafanya vizuri katika mashindano ya kimataifa ndani na nje ya nchi, kuongezeka kwa idadi ya wakuzaji wa mchezo wa ngumi, kuongezeka kwa mapambano 35 ambayo yamefanyika kati ya Aprili, 2019 hadi Machi, 2020.
Fauka ya hayo, wadhamini kujitokeza kuwekeza katika kusimamia na kuhakikisha haki za mabondia zinazingatiwa ikiwemo kupitiwa kwa mikataba yao ya mapigano kabla ya pambano pamoja na kuimarika kwa mahusiano ya vyombo vya kusimamia michezo katika nchi tofauti pamoja na vyama vinavyoshindanisha mikanda tofauti duniani ikiwemo, WBO, WBA, WBC, ABU na UBO.
Hatua hiyo imesaidia wanachama wa Ngumi za kulipwa waliosajiliwa kwa muda wa miaka mitatu kuanzia 2016 hadi 2019 kufikia 22, taswira ambayo inaonesha kuongezeka kwa mwamko wa kuanzisha na kusajili vikundi vya sanaa na michezo nchini.
Kulingana na takwimu hiyo, kati ya vikundi 22, vikundi 17 vinajihusisha na mchezo wa ngumi, sanaa na michezo mingine wakati vikundi vitano tu vilivyoanzishwa na kusajiliwa vinajihusisha na mchezo wa ngumi pekee.
Kwa hakika jambo hili linaonesha wazi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imetekeleza agizo la CCM katika ilani yake iliyotolewa wakati wa uchaguzi wa 2015 kwani kwa takwimu hizo ni kweli Serikali kwa kishirikiana na sekta binafsi imeweza kuanzisha vituo vya kuendeleza vipaji vya wanamichezo mahiri na kutumika kama vituo vya maandalizi ya wanamichezo wanaoiwakilisha Tanzania katika michezo ya kimataifa.
Kwa mantiki hiyo, mwandishi wa makala hii amebainisha kuwa mwamko wa kuanzisha michezo shirikishi ni mkubwa zaidi kuliko mchezo mmoja mmoja na hatua hii Serikali inapaswa kupongezwa kwani chanda chema huvishwa pete.
Kwa nafasi mafanikio haya na nafasi hii, mwanamichezo anayeshriki katika mchezo wa ngumi akiwa katika kikundi mazoezi (gym) anayonafasi kubwa zaidi ya kuwa mwanamasumbwi bora zaidi ya yule ambaye yupo kweye masumbwi pekee.
Hatua hiyo inamsaidia mwanamichezo kuwa bora katika mchezo katika kikundi ambacho kinahusisha mchezo zaidi ya mmoja ana fursa ya kupata vifaa vinavyomsaidia kufanya mazoezi ya uhakika, utimamu wa mwili na kupata msaada wa kitaalamu katika mchezo husika kutoka kwa walimu mbalimbali wanaokuwepo wakati wa mafunzo na mazoezi yanayompa motisha unaompelekea kuwa mwanamichezo bora.
Hakika Kamisheni ya Kusimia Ngumi za Kulipwa imekuwa mwarobaini wa mchezo huo ambapo migogoro ya mara kwa mara imekuwa ni historia ikiwemo mapromota kuvamia tasnia hiyo na kuharibu mustakabali mzuri wa mchezo huo nchini.
Ni ukweli usiopingika, kila lenye mafanikio halikosi kuwa na changamoto, mchezo wa ngumi za kulipwa bado unakabiliwa na changamoto ya kutokuwepo kwa makocha wenye viwango vya kimataifa wenye nyota zinazotakiwa, vifaa vya kufanyia mazoezi, uhaba wa wadhamini pamoja na maeneo ya kufanyia mazoezi na ulingo unaotumika wakati wa mashindano. Kwa hakika Serikalia ya Awamu ya Tano itaendelea kuzitatua changamoto zote zilizosalia na kwa hakika mambo yatakuwa mazuri hivi punde.
Mafanikio haya yaliyofikiwa ni makubwa mno kwa mchezo huu ulionza kuchezwa hata kabla nchi yetu haijatawaliwa na wakoloni katika karne ya 19. Mchezo huu ulichezwa katika viwanja vikubwa vyenye mikusanyiko mikubwa ya watu (Coliseum) huko Roma na (Arena) huko Athina, iliyokuwa katika hekalu kubwa la ufalme wa Wayunani (Ugiriki) la Akropolis. Viwanja hivyo vilikuwa ndio mwanzo wa ulingo wa kisasa kwani japokuwa ulingo wa kisasa ni wa mraba lakini mwanzo wake ni Arena ya mduara.
Mwisho.