Friday, September 6, 2019

Kambi Ya Kitaaluma Kwa Wanafunzi Wa Kidato Cha Nne Wenye Ufaulu Hafifu Yazinduliwa Simiyu

Na Stella Kalinga, Simiyu RS
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amezindua rasmi kambi ya kitaaluma ya siku 60 kwa wanafunzi wa kidato cha nne waliopata ufaulu hafifu (daraja sifuri) katika mtihani wa 'Mock', lengo likiwa ni kuwasaidia waweze kuongeza ufaulu wao katika mtihani wa Taifa utakaofanyika mwezi Novemba 2019.

Akizindua kambi hiyo Septemba 05, 2019 Mtaka amesema wanafunzi hao watafundishwa masomo manne tu ambayo ni Kiswahili, Kiingereza ,Uraia(Civics) na Historia, hivyo akatoa wito kwa walimu mahiri waliochaguliwa kuwafundisha wanafunzi hao kwa moyo na upendo ili wanafunzi hao waweze kupata alama D na kuendelea katika mtihani wa Taifa.

"Hawa watoto wafundisheni masomo manne, Kiswahili, Kiingereza, Historia na Civics; wafundisheni kwa moyo, wapeni mazoezi ya mara kwa mara katika siku hizi 60 watakazokuwa kambini, muwasaidie watoke kwenye F wapate angalau D nao wapate vyeti, kwa sababu hata ajira siku hizi kigezo ni angalau mtu awe na cheti cha kidato cha nne" alisema Mtaka.

Katika hatua nyingine Mtaka ametoa wito kwa jamii ya Simiyu kuendelea kuwekeza kwenye elimu ili kuuwezesha mkoa kushindana kiuchumi kwa kuwa maendeleo ya kiuchumi yanategemea maendeleo ya elimu katika eneo husika.

Afisa Elimu mkoa wa Simiyu, Mwl.Ernest Hinju amesema kati ya Wanafunzi 9956 waliofanya mtihani wa  Utimilifu (Mock), 1300 hawakupata alama D hata moja, hivyo waliopata matokeo hafifu (daraja sifuri) wamewekwa pamoja wafundishwe masomo manne ili waweze kuongeza ufaulu katika mtihani wa Taifa, huku waliopata daraja la kwanza hadi la nne wakiendelea na kambi kufundishwa masomo yote.

Aidha, Hinju ameongeza kuwa  kambi za kitaaluma zimechangia kuongeza ufaulu kwenye Mtihani ya Taifa wa darasa la saba, kidato cha nne na kidato cha sita, ambapo katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2016 ufaulu ulikuwa asilimia 74 mkoa ukiwa nafasi ya 14 kati ya mikoa 26, mwaka  2017 ufaulu asilimia 79.8 nafasi ya 11 na mwaka 2018 ufaulu asilimia 82.5  ukashika nafasi ya 9 kati ya mikoa 26.

Kwa upande wao wanafunzi wa kidato cha nne waliopo kambini  wameshukuru kuwekewa kambi hiyo na wakaeleza imani yao juu ya uwepo wa kambi hiyo ambapo wameomba kambi za kitaaluma Simiyu ziwe endelevu ili ziwasaidie kujifunza na kujiandaa vema na mitihani ya Taifa hatimaye mkoa uweze kufanya vizuri.

"Tunawashukuru viongozi wetu na wazazi wetu kwa kukubali kutuwekea kambi ya kitaaluma, ninashauri kambi hizi zisiishie kwetu ziendelee na kwa wadogo zetu ili mkoa wetu uweze kuongeza ufaulu" alisema Esther Nashoni mwanafunzi shule ya sekondari Bariadi(Bariadi)

Mkuu wa Shule ya Sekondari Simiyu, Mwl.Paul Susu amesema walimu wamejiandaa vema katika kuwafundisha wanafunzi na kuwapa mitihani ya mara kwa mara ili waweze kufanya vizuri, huku akitoa wito kwa wadau mbalimbali wa elimu kujitolea katika ujenzi wa miundombinu ya elimu ili kuwe na miundombinu ya kutosha itakayoongeza nafasi kwa kambi za kitaaluma kufanyika  vizuri.

Kambi ya kitaaluma kwa wanafunzi wa Kidato cha nne iliyozinduliwa Septemba 05, 2019 ilianza rasmi Septemba Mosi na inatarajiwa kufanyika ndani ya siku 60 kabla ya kufanya Mtihani wa Taifa mwezi Novemba.

MWISHO



Source
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...