Tuesday, April 2, 2019

MAJAMBAZI WANYOFOA MASHINE YA ATM KWA TINGATINGA

Majambazi wamenyofoa na kutokomea na mashine ya kielektroniki ya kutolea pesa nchini Ireland ya Kaskazini.

Majambazi hao walitumia tingatinga ambalo pia waliliiba katika kunyofoa ATM hiyo kutoka kwenye ukuta wa duka moja katika Kaunti ya Antrim.

Tukio hilo limetokea saa tisa ya usiku wa Jumatatu. Polisi wamethibitisha kuwa jengo hilo limeharibiwa vibaya.

Mmiliki wa duka hilo Walter Millar amesema kuwa ATM hiyo "itakumbukwa sana" na jamii ya eneo hilo na sasa kuna "hofu" juu ya kupatiwa mashine nyingine baada ya wizi huo.

Awali alipopokea taarifa juu ya wizi huo, mmiliki wa duka hilo bwana Millar alidhani ni uzushi tu wa Siku ya Wajinga, Aprili mosi.

"Nachoweza kusema ni kuwa, wametumia tingatinga ambalo waliliiba kwenye eneo moja la ujenzi mwishoni mwa mtaa, wakainyofoa mashine na kuipakia kwenye gari na kuondoka nayo," amesema.

"Ukuta wa jikoni umeharibiwa kabisa...tumekuwa na wakati mgumu, na ukijumlisha na hali ya kiuchumi iliyopo, vitu kama hivi vinatumaliza kabisa."Mmiliki wa duka Walter Millar awali alihusisha taarifa za tukio hilo na Siku ya Wajinga, Aprili 1.

Majambazi wa ATM

"Tulipokea simu kuhusu tukio hilo mishale ya saa 9:25 usiku kuwa tingatinga linaungua moto nje ya duka ambalo ATM imechomolewa," Inspekta wa Polisi Richard Thornton amesema.

"ATM imenyofolewa ukutani na kuharibu jengo ilipokuwa imewekwa...tunawataka mashuhuda wajitokeze, hususan walioiona gari ya rangi ya fedha."

Mwezi uliopita, polisi walitangaza kuundwa kwa kikosi kipya cha kupambana na wizi wa mashine za ATM.

Toka ulipoanza mwaka 2019, mashine saba za ATM zimeibiwa. Polisi pia wanaamini kuna makundi kadhaa ya majambazi ambayo yanajihusisha na wizi wa mashine hizo.

Wamiliki wa maduka sasa wanaonesha uoga wao juu ya kuweka mashine hizo kwenye maeneo yao ya biashara na tayari watu kadhaa wametahadharisha endapo wizi huo utaendelea basi watalazimika kuzitoa mashine hizo.
Chanzo - BBC
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...