Na. Alex Sonna,Dodoma
Jeshi la polisi mkoa wa Dodoma linawashikilia watuhumiwa 29 wakiwemo makahaba 22 waliokuwa wakifanya biashara ya ngono, wanaume watano waliokuwa wakinunua pamoja na wamiliki wanne wa maeneo yanayoruhusu biashara hizo.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo Kamanda wa polisi Mkoa wa Dodoma Gilles Muroto,amesema kati ya watuhumiwa hao wanawake ni 22 na wanaume wa tano pia limewakamata wamiliki wanne wa maeneo yanayodaiwa kuruhusu kufanyika kwa ukahaba.
"Katika Operesheni hiyo wahalifu wanaofanya makosa ya udhalilisha wa utu dhidi ya Maadili tumewakamata watuhumiwa 29, Makahaba 22, wanaume watano watano na wamiliki wanne wa maeneo ambayo yanaruhusu kufanyika kwa biashara ya ukahaba ," amesema Muroto.
Kamanda Muroto amesisitiza kuwa biashara hiyo haitakiwi katika Jiji hili kwani kuna kazi nyingi za kufanya ili kujipatia kupata na si kuuza miili yao ambayo ni kinyume cha sheria ya kanuni ya adhabu sura 16 kifungu cha 146 hivyo watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Katika tukio lingine jeshi la polisi limewakatama wahamiaji haramu wanne walioingia nchini bila kibali wakitokea mkoani Arusha kwenda mkoani Mbeya.
Kamanda Muroto amesema kuwa wahamiaji hao walikamatwa oktoba 6,2018 ambapo wawili walikamatwa katika kizuizi cha polisi Zamahero wilaya ya Bahi , huku wengine walikamatwa katika eneo la nane nane jijini hapa.
Kamanda Muroto amewataja Waliokamatwa Wilayani Bahi ni Abdi Mussa (26) raia wa Somalia na Migafu Gezehani (18) raia wa Ethiopia wakisafiri na basi la HAJI's LINE UP lenye namba za sajili T. 298 DCH kutoka mkoani Arusha kwenda Mkoani Mbeya
"Waliokamatwa katika eneo la nane nane stendi kuu ya mabasi jijini Dodoma ni Abdi Mohamed na Mohamed Dai wote raia wa Solalia. Watuhumiwa hao tutawafikisha mahakamani pindi upelelezi utakapokamilika," amesema Muroto.
Katika Operesheni hiyo kamanda amesema kuwa jeshi hilo limemkamata Malogo Sanja (41) mkazi wa wilaya ya Mpwapwa akiwa na silaha aina ya gobole likiwa na risasi 16 ambazo ni vipande vya nyama vilivyotengezwa kienyeji.
"Silaha hiyo imekutwa ikitumika katika matukio mbalimbali ya kiuhalifu kama uwindaji haramu na unyang'anyi.Pia mtuhumiwa huyo alikutwa na bhangi kilo tatu na nusu pamoja na mbegu za bhangi kilo tano," amesema Muroto.
Kwa mujibu wa kamanda Muroto Operesheni ya vunja vijiweni katika mkoa wa Dodoma pia imekamata Luckas Andambile (42) mkazi wa Mbeya kwa kujifanya Askari na kufanya utapeli wa kiasi cha shilingi 60,000.
Wakati huo Jeshi hilo linawashikilia watu 10 kwa tuhuma za kushiriki tukio la kuchoma nguzo za umeme wa rea katika kijiji cha Makang'wa wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma.
Kamanda Muroto amesema kuwa Operesheni hiyo waliitkeleza kuanzia oktomba 3 hadi 9, 2018 ambapo watuhumiwa wote watapandishwa mahakamani pindi Upelelezi wa matukio hayo utakapokamilika.