Tuesday, October 9, 2018

Mara: Mchungaji Afariki Dunia wakati Akimwombea Marehemu!


Mchungaji wa Kanisa la Evangelist Assemblies of God Tanzania (EAGT) la Sirari, tarafa ya Inchugu wilayani Tarime mkoani Mara, Nestory Papaa amefariki dunia wakati akimwombea marehemu katika mji wa Kehancha nchini Kenya.


Taarifa za kuaminika zimesema mchungaji huyo alikwenda katika mji huo na rafiki zake ili kuhani msiba wa shemeji wa rafiki yake.

Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa maziko ya mchungaji huyo, Diwani wa Kata ya Sirari ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Mpakani, Nyangoko Paulo, amesema mchungaji huyo alifikwa na umauti baada ya kuanguka ghafla wakati akimuombea marehemu huyo.

Ndugu wa Mchungaji huyo aliyejitambulisha kwa jina Charles Papaa alisema kaka yake aliyekuwa Mchungaji wa Kanisa la EAGT lililopo katika mji wa Sirari na pia mfanyabiashara wa duka la kuuza vipodozi alikufa katikati ya maombezi aliyokuwa akiyafanya.

Mnamo Jumatano iliyopita, kaka na marafiki zake akiwemo Nyangoko Roman walikwenda kuhani msiba wa shemeji yake na Nyangoko huko Kehancha, Kenya.

Wakati akitoa neno ghafla aliishiwa nguvu na kuanguka chini ambapo watu waliokuwa msibani hapo na marafiki zake walijitahidi kumkimbiza katika hospitali ya jirani ya Migori ili kumpatia matibabu, lakini alipoteza maisha kabla ya kupatiwa matibabu,” amesema Charles.

Alisema wakati wa uhai wake Mchungaji Papaa alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa moyo na taarifa ya madaktari katika hospitali alikokimbizwa baada ya kuanguka zinaeleza kuwa kifo chake kimesababishwa na mshituko wa moyo.

Alisema Mchungaji huyo alizikwa Jumamosi katika Kitongoji cha Buriba kata hiyo ya Sirari.

Katika tukio lingine, mkazi wa Kitongoji cha Nyamorege kata hiyo ya Sirari ambaye ni mwendesha bodaboda, Sinda Gichengwe maarufu kwa jina la Mtandao amekufa baada ya kuchomwa kisu mgongoni.

Sinda anadaiwa kuchomwa kisu na mtu aliyefahamika kwa jina moja la Samweli mwenyeji wa Mugumu, Serenngeti usiku wa kuamkia Oktoba 7, mwaka huu. Tukio hilo lilitokea katika Baa ya Migombani wakati wawili hao wakigombea mwanamke.

Imedaiwa kuwa baada ya kufanya kitendo hicho mtuhumiwa alitoroka. Kamanda wa Poliisi Kanda Maalumu ya Tarime /Rorya, Henry Mwaibambe amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema Jeshi la Polisi linamsaka mtuhumiwa huyo ili aweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Source: Habari Leo
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...