Friday, August 13, 2021

WACHAWI WAZUA GUMZO BAADA KUTUPA JENEZA LENYE VITU VYA AJABU MLANGONI

Wenyeji wa kijiji cha Karando nchini Kenya wameingiwa na hofu baada ya kuamka asubuhi na kukuta jeneza lililokuwa na kuku na rozari likiwa limetupwa katika nyumba ya mmoja wao.

Wenyeji hao waliamkia kisa hicho mnamo Alhamisi, Agosti 12,2021 asubuhi. Kando na kuku aliyekuwa hai na rosari, jeneza hilo pia lilikuwa na konokono na vitu vingine vya ajabu.

Mmiliki wa boma hilo Silvestor Okero alisema waliamka asubuhi na kupata jeneza hilo likiwa limetupwa nyumbani kwake.

Okero aliingiwa na wasiwasi na kumwita mmoja wa majirani zake aje kushuhudia kile alichokiona nyumbani kwake.

"Jeneza lilikuwa limefungwa kwa hivyo sikulifungua lakini nikampigia mmoja wa majirani zangu aje kunisaidia kuhusiana na suala hilo zito," Okero alisema.

Mwanaume huyo alisema maishani mwake hajawahi kushuhudia vituko kama hivyo namkuongeza kwamba amekuwa akiishi kwa amani na watu na wala hana uadui wowote na yeyote.

"Sina tatizo lolote na mtu yeyoye lakini nashuku huenda kisa hiki kimetekelezwa na mmoja wa jamaa zangu ambaye tunazozania shamba," aliongeza.

Mmoja wa majirani zake alisema kwamba alikwenda nyumbani humo alipopigiwa simu, akaona jeneza, na kuripoti jambo hilo kwenye kituo cha polisi cha Riat; jeneza hilo baadaye lilifunguliwa.

Alidokeza kwamba wenyeji waliliondoa jeneza hilo bomani mwake na kisha wakaliteketeza na tunguri zilizokuwa ndani. Wakazi hao walishuku huenda kikawa ni kisa cha uchawi na kuwataka maafisa wa polisi kuanzisha uchunguzi.

Walilalamikia kuongezeka kwa visa vya uchawi katika eneo hilo, wakisema vimelemaza maendeleo na kuwanyima usingizi.

CHANZO - TUKO NEWS

Source

Kumekucha..Sabaya Awataja Magufuli, Dk Mpango na Gavana BoT Kuwa Walifahamu Operesheni Aliyokuwa Akiifanya Arusha.



Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya amewataja Hayati John Magufuli, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango na Gavana wa Benki Kuu kuwa walikuwa wanajua operesheni aliyokuwa akiifanya Arusha.

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya leo Ijumaa Agosti 13, 2021 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha amewataja Hayati John Magufuli, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango na Gavana wa Benki Kuu kuwa walikuwa wanajua operesheni aliyokuwa akiifanya Arusha.

Sabaya amesema hayo wakati akitoa utetezi mbele ya Hakimu mkazi mwandamizi Odira Amworo kuwa alichokuwa anakifanya Arusha Februari 9, 2021 haikuwa operesheni yake ya kwanza kuagizwa na hayati Rais Magufuli 

Diwani wa CCM aangua kilio mahakamani akisimulia namna Sabaya alivyomtisha kwa bastol

Akiongozwa na Wakili anayemtetea Mosses Mahuna, wakati alipoanza kujitetea mahakamani hapo amesema kesi hiyo ni ya kutengeneza na yeye hajaiba wala kumtishia mtu yoyote kwa silaha.

Sabaya alisema siku ya tukio Februari 9, 2021 alipomaliza kuongoza kikao cha kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Hai, alipokea simu ya Dk Magufuli aliyemwelekeza kazi ya kufanya katika mkoa wa Arusha ambapo pia alipaswa kuwapitia watu wengine wanne katika uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), ambapo watu hao walikuwa na maelekezo juu ya kazi hiyo wanayoenda kufanya.

"Hiyo haikuwa kazi ya kwanza kwa sababu miezi michache iliyopita tulipewa zoezi la kukamata mitambo inayotengeneza noti bandia na tulifanikiwa kukamata mitambo na fedha Sh 800 Milioni bandia eneo la Chanika wilaya ya Temeke mkoa wa Dar es Salaam ,Gavana wa BoT anajua na aliyekuwa Waziri wa Fedha kwa wakati huo Dk Philip Mpango, Makamu wa Rais wa sasa pia anafahamu,"

IGP Sirro akemea wanaojihusisha na dawa za kulevya



Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro ameitaka jamii kujiepusha na kuacha vitendo vya udhalilishaji na biashara ya dawa za kulevya kwani vyombo vya dola vitatumia sheria zilizopo kuwashughulikia wanaojihusisha na vitendo hivyo.

IGP Sirro amesema hayo leo wakati akifunga mafunzo ya uongozi mdogo wa Cheo cha Sajenti wa Polisi yaliyofanyika kwa muda wa miezi miwili katika Chuo cha Polisi Zanzibar ambapo jumla ya wahitimu 1297 walihitimu mafunzo hayo na kupandishwa vyeo.

Kina Mbowe waigeuzia kibao Serikali, Hakimu atoa agizo



Freeman Mbowe akiwa mahakamani Kisutu
KIONGOZI wa Chama Kikuu cha Upinzani Tanzania-Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu, wameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, iwasilishe ombi lao Mahakama Kuu ya Tanzania la kupinga matamshi yaliyotolewa na Taasisi ya Serikali, dhidi ya mashtaka ya kula njama za kufanya ugaidi yanayowakabili mahakamani hapo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Ombi hilo limewasilishwa mahakamani hapo leo Ijumaa, tarehe 13 Agosti 2021 na mawakili upande wa utetezi, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Thomas Simba.

Akiwasilisha ombi hilo, Wakili upande wa utetezi, Peter Kibatala, amedai matamshi hayo ambayo hakuyataja, yataathiri mwenendo wa kesi hiyo.

Amedai, wateja wake wanayaona matamshi hayo kama hukumu, hivyo hawana imani kama mashtaka yao yataendeshwa kwa uhuru mahakamani.


"Tumeleta taarifa ya kusudio la kuiomba mahakama ipeleke Mahakama Kuu kama suala la kikatiba, matamshi yaliyotolewa na taasisi fulani hapa nchini, watu wote wanaifahamu, wamesikia.

"Tunachosema maneno yale au matamshi yale kwa maoni yetu sisi na wateja wetu, yameingilia uhuru wa mahakama. Sio mahakama hii tu, lakini mahakama itakayokwenda kusikiliza shauri la ugaidi linalowakabili washtakwia," amedai Kibatala.

Katika maombi hayo, Mbowe na wenzake, wanaiomba Mahakama Kuu iangalie kama matamshi hayo yameingilia uhuru wa mahakama na kama itabainika yameingilia uhuru wa mhimili huo, kesi husika ifutwe.


"Kwa kuwa mamlaka ile yenye nguvu naishawishi basi matamshi yale kwa namna yalivyotamkwa, yamewafanya wateja wetu kuona tayari wamehukumiwa na kwamba hakuna namna yoyote wanaweza wakapata fair trial, tumeomba iangalie matamshi yale kama yameingilia uhuru wa mahakama," amesema Kibatala.

Kibata ameongeza "na iwapo au la matamshi yale yamesababisha kesi isiwe na mantiki tena na hakuna la kufanya isipokuwa kufutwa."

Kibatala amesema hayo nje ya Mahakama hiyo baada ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba kuahirisha kesi hiyo hadi tarehe 27 Agosti 2021.

Awali, Wakili wa serikali Pius Hilla, alisema kesi imekuja kwa ajili ya kutajwa lakini washtakiwa wameshinmdwa kufikishwa mahakamani kutokana na kukosekana usafiri jambo lililopingwa na Kibatala, akisema walipaswa kuletwa mahakamani na si kama walivyofanya.

STEVE NYERERE : MSISIKILIZE WAPOTOSHAJI KUHUSU CHANJO KACHANJENI



Na Magrethy Katengu - Dar es salaam
Wanzania wamehimizwa kupuuza maneno ya upotoshaji yanayoenezwa kwenye mitandao ya kijamii na baadhi ya wanasiasa na watu maarufu viongozi wa dini kuhusu chanjo ya UVIKO -19.

Wito huo umetolewa leo na Balozi wa uhamasishaji wa chanjo ya UVIKO 19 ambaye pia mwenyekiti wa taasisi ya Wazalendo kwanza Steve Mengele Nyerere wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam ambapo amesema wapo watu wanahamasisha wananchi kutokuchanja kwa kueleza madhara ambayo siyo ya kweli.

"Ukifanya ubishi wa hili jambo fanya mwenyewe usiwashawishi wengine kaa kimya nyumbani kwako kwakuwa ukibainika unanashawishi watu wasichanje usijutie mdomo wako",alisema Steve.

Aidha amewahimiza vijana ambao ndio taifa la kesho kuwekeza nguvu zao katika kulisaidia Taifa kukua kiuchumi na sio kujiingiza kwenye makundi ya mitandao jamii inayolenga kuchafua serikali na kurudisha nyuma jitihada za Rais Samia ambaye amejielekeza katika kujenga uchumi na kusaida jamii kujikwamua katika lindi la umasikini.

Kwa upande wake Asha Baraka ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kujali wananchi wake Kwa kuwaletea  chanjo na kuigawa bure kwa kila mmoja ili kusaidia hata wasio na uwezo wapate chanjo

Aidha Wazalendo kwanza wanasisitiza kuwa ugonjwa wa UVIKO -19 upo na unaua hivyo bi muhimu wananchi waliopo kwenye kundi la umri waliopewa kipaumbele kujitokeza na kuchanjwa kwa hiyari zao ili kunusuru maisha yao dhidi ya ugonjwa huo.

Source

Mwenyekiti wa Kampuni za Asas Group, Alhaj Faraj Ahmed Abri Afariki Dunia


Mwenyekiti wa Kampuni za Asas Group, Alhaj Faraj Ahmed Abri amefariki dunia leo Ijumaa Agosti 13 alfajiri, akiwa jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika familia hiyo, Mzee Abri atazikwa leo baada ya Swala ya adhuhuri katika makaburi ya Kisutu Dar es Salaam.

"Hakutakuwa na mikusanyiko kwa tutakaokuwa Iringa, tafadhali tutumie zaidi teknolojia za habari kutoa pole na shughuli nyingine," imeeleza taarifa hiyo.



Source

ULEGA ATAKA MIGOGORO YA WAKULIMA NA WAFUGAJI KUKOMESHWA NCHINI

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akizungumza na viongozi wa Wilaya ya Handeni, Mkoani Tanga (hawapo pichani) mara baada ya kufika katika wilaya hiypo kwa ziara ya kikazi ya siku moja, Mkoani Tanga. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi).

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akizungumza na viongozi wa Wilaya ya Handeni, Mkoani Tanga na kutoa maagizo ya kukomeshwa kwa migogoro baina ya wakulima na wafugaji kote nchini, mara baada ya kufika katika wilaya hiyo kwa ziara ya kikazi ya siku moja.  (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi).


Na. Edward Kondela

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amewataka viongozi wa maeneo mbalimbali nchini kuanzia ngazi ya kijiji kuhakikisha wanasimamia haki na amani na kujiepusha na vitendo vya rushwa ili kudhibiti migogoro ya wakulima na wafugaji.

 

Naibu Waziri Ulega amebainisha hayo (12.08.2021) wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga na kuibainisha hayoa kwenye kikao chake na uongozi wa wilaya hiyo na kuwataka pia wataalam wa sekta ya mifugo washirikiane vyema na viongozi katika kutoa pia elimu juu ya umuhimu wa makundi hayo mawili ya wakulima na wafugaji.

 

Mhe. Ulega amesema wafugaji lazima waishi kwa upendo maeneo walipo pamoja na wafugaji wengine na wakulima kwa kuwa ni dhambi kubwa kuchukua mifugo na kuingiza kwa makusudi kwenye shamba la mkulima.

 

"Kitendo cha ng'ombe kupelekwa kwenye mashamba ni jinai kama jinai nyingine siyo haki kwa mkulima au mfugaji kuchukua hatua kinyume na taratibu na viongozi wa kijiji wawe wasimamizi wa haki na amani na wasifanye upendeleo pamoja na kufanya vitendo vyovyote vya rushwa." amesema Mhe. Ulega

 

Naibu Waziri Ulega amelazimika kutoa maelekezo hayo baada ya kupokea taarifa ya uongozi wa Wilaya ya Handeni kuwa kumejitokeza migogoro baina ya wakulima na wafugaji hadi kusababisha vifo vya baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo hali ambayo imekuwa ikisababisha hofu ya mahusiano baina ya makundi hayo mawili.

 

Katika taarifa hiyo wameiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha inaweka mikakati mbalimbali ya kukomesha migogoro hiyo ambayo imekuwa ikisababisha hofu, ukizingatia Wilaya ya Handeni ina mifugo mingi na imekuwa ikifanya biashara ya kupeleka mifugo ndani na nje ya nchi.

Chama kujiunga na Klabu ya RS Berkane ya Morocco


CLATOUS Chama kiungo namba moja kwa kutengeneza pasi za mwisho anatajwa kujiunga na Klabu ya RS Berkane ya Morocco kwa dili la miaka mitatu.


Timu hiyo inanolewa na Kocha Mkuu, Florent Ibenge ambaye alikuwa anafundisha AS Vita anatambua vema uwezo wa Chama kwa kuwa alikutana naye kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita.

Ndani ya Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2020/21 nyota huyo alitengeneza jumla ya pasi 15 na alifunga mabao nane akiwa ni namba moja kwa utengenezaji wa pasi ndani ya ligi.

Taarifa zimeeleza kiungo huyo hatakuwa sehemu ya kikosi cha Simba kwa msimu ujao wa 2021/22.

Mbali na Chama pia nyota wao Luis Miquissone yupo kwenye hesabu za mwisho kutua nchini Misri kwa ajili ya kujiunga na Klabu ya Al Ahly ya Misri.

Tayari jezi namba 11 ambayo aliyokuwa anavaa Luis amekabidhiwa kiungo mpya Peter Banda ambaye anatajwa kuwa mbadala wa nyota huyo.

Simba imeweka kambi nchini Morocco kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao wa 2021/22 ambapo Luis hakuwa sehemu ya kikosi hicho ambacho kipo kambini.

 

Serikali ya Canada kuanzisha kutoa hati ya chanjo kwa ajili ya safari za kimataifa

 Waziri wa Uraia na Uhamiaji wa Canada Marco Mendicino, alitangaza kuwa wale ambao wamechomwa dozi mbili za chanjo dhidi ya corona (Kovid-19) watapewa hati ya chanjo itakayotumika katika safari za kimataifa.

Mendicino, ambaye hakutoa tarehe halisi, alisema kuwa mpango huo utatekelezwa katika siku za kwanza za msimu wa vuli.

Akielezea kuwa serikali yake inafanya kazi na nchi zingine kutambua hati za chanjo, Mendicino alisema kuwa watu wa Canada waliopata chanjo kikamilifu wataweza kupata hati ya serikali ambayo itathibitisha historia yao ya chanjo ya Kovid-19 kwa sababu za kusafiri kimataifa.

Mendicino pia alisisitiza kuwa hati ya chanjo itakayotolewa itajumuisha data juu ya aina, tarehe na mahali pa chanjo zilizotolewa, na kubainisha kuwa utumiaji wa hati iliyoandaliwa kwa safari za kimataifa baina ya nchi imeachwa kwa uamuzi wa serikali za majimbo.

Mfumo wa hati ya chanjo, ambao unaendelea kutumika Bulgaria, Jamhuri ya Czech, Denmark, Ujerumani, Ugiriki, Croatia na Poland, pia ulianzishwa huko Japan mnamo Julai.

Wale wanaotumia programu ya ArriveCAN, ambayo Canada ilizindua mnamo Julai, wameondolewa ulazima wa kukaa karantini wanapoingia nchini ikiwa watathibitisha maelezo yao na kujaza data zinazohitajika kwenye programu.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...