Monday, March 3, 2025

ELIMU YA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA TAIFA GAS NA BARRICK YAENDELEA KUWAFIKIA WANANCHI


Mkufunzi kutoka kampuni ya Taifa Gas,Praygod Ole Naiko akionesha kwa vitendo matumizi ya jiko la gesi kwa washiriki wa mafunzo
Mmoja wa washiriki akionesha matumizi ya jiko la gesi kwa vitendo baada ya kuhitimu mafunzo
Mwakilishi wa Barrick, Mary Lupamba akiongea na washiriki wakati wa mafunzo hayo
Washiriki wa mafunzo wakiimba kwa furaha wakati wa mafunzo
Baadhi ya washiriki wakipokea vyeti vya ushiriki wa mafunzo hayo
Baadhi ya washiriki wakipokea vyeti vya ushiriki wa mafunzo hayo
Picha ya baadhi ya washiriki wa mafunzo wakiwa na wakufunzi baada ya kukabidhiwa vyeti vya ushiriki

****
Wakati Maadhimisho ya  Wiki ya Wanawake Duniani yakiendelea, kampuni ya Taifa Gas kwa kushirikiana na Barrick imeendelea kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan za kupambana na utunzaji wa mazingira kupitia nishati safi ya kupikia kwa kutoa mafunzo ya matumizi ya nishati salama ya kupikia kwa Wananchi.

Akiongea wakati wa kuhitimisha mafunzo ya siku 3 yaliyofanyika wilayani Kahama na kuwashirikisha wananchi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Mkufunzi kutoka kampuni ya Taifa Gas, Praygod Ole Naiko amesema mafunzo haya yatasaidia kueneza elimu ya matumizi ya nishati safi ya gesi kwenye jamii.

"Jitihada hizi ni kuhakikisha kwamba mapinduzi ya kijani yanafanikiwa kwa watanzania wengi zaidi kuanza kutumia nishati safi kwa ajili ya kupikia ili kuchochea utunzaji wa mazingira sambamba na ukuaji na Uchumi kwa ujumla," amesema Ole Naiko.

Amesema dhamira ya Taifa Gas ni kuunga mkono agenda ya nishati safi inayoongozwa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan juhudi hizo zinaendana na uongozi wake wenye maono na kujitolea kwa Mheshimiwa Rais katika mandhari nzima ya nishati safi nchini.

Kwa upande wake ,Mwakilishi wa Barrick, Mary Lupamba, akiongea kuhusu mafunzo hayo yatakayoendelea kutolewa kwa Wananchi kupitia ushirikiano huo amesema Barrick inajivunia kuwa sehemu ya program hii ya mafunzo ya Nishati safi kwa Wananchi na inaamini yatafanikisha kuleta mabadiliko chanya kwa walengwa na jamii nzima kwa ujumla.

Akiongea kwa niaba ya Washiriki wa mafunzo hayo,mmoja wa washiriki, Amina Juma amesema wamenufaika kujua umuhimu na faida za matumzi ya nishati ya gesi sambamba na kujua usalama wa matumizi ya nishati hiyo na kuondoa dhana iliyojengeka kuwa nishati hiyo ina gharama kubwa.

Naye mshiriki Joseph Musa mkazi wa kitongoji cha Kakola amesema kuwa kupitia mafunzo hayo ambayo yamehusisha Wanawake na Wanaume wameweza kupata elimu ya undani wa matumizi ya nishati salama na alishukuru Taifa Gas na Barrick kwa kupeleka elimu hii katika maeneo ya vijijini ambako Wananchi wengi wanatumia nishati za mkaa na kuni ambazo si salama kwa mazingira na afya.

Elimu ya matumizi ya nishati safi ya Taifa Gas na Barrick inayoendelea kutolewa katika jamii ni mwendelezo wa kampeni ya kufikisha elimu hii kwa wananchi iliyoanza mwaka jana wakati wa maadhimisho ya kupinga ukatili wa kijinsia ambapo wananchi kutoka mikoa mbalimbali nchini walifikiwa na elimu hii.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...