Monday, March 3, 2025

SHACMAN NA CFAO MOBILITY KUIMARISHA SEKTA ZA VIWANDA NA USAFIRISHAJI TANZANIA


CFAO Mobility Tanzania imezindua rasmi usambazaji wa malori ya Shacman katika soko la Tanzania, hatua inayolenga kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya magari ya kazi nzito yenye uimara na ufanisi mkubwa. Hafla ya uzinduzi huo ilifanyika Februari 27, 2025, katika viwanja vya The Green Grounds, Oysterbay, Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Hassan Serera, pamoja na wadau muhimu wa sekta hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Suleiman Hassan Serera aliukaribisha ujio wa Shacman na kusisitiza mchango wake katika kukuza sekta za miundombinu, madini, na usafirishaji nchini Tanzania.

"Uzinduzi huu leo si tu kuongeza chapa nyingine maarufu sokoni, bali ni hatua muhimu katika kuboresha ufanisi, uimara, na uhakika katika mnyororo wa faida kwenye sekta za viwanda na usafirishaji. Tanzania inatekeleza miradi mikubwa ya miundombinu, upanuzi wa migodi, na kuboresha njia za biashara, hivyo Shacman imekuja kwenye wakati muafaka. Uchumi wetu unakua kwa kasi, na sekta za usafirishaji na viwanda ni nguzo muhimu katika ukuaji huo. Malori mazito si magari tu—ni injini zinazochochea maendeleo." Alisema Dkt. Serera.

"Zaidi ya kuleta malori ya kisasa, hatua hii inafungua milango kwa ukuaji wa teknolojia, uundaji wa ajira, na kuimarisha uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na China." Aliongeza.
Kwa kuwa CFAO Mobility Tanzania ni msambazaji rasmi, biashara mbalimbali sasa zinaweza kupata modeli bora za Shacman, ikiwa ni pamoja na Tractor Horse - H3000S 6X4 (400HP) model SX4255HU324R na Dump Truck - H3000S 6x4 (340HP) model SX3255MR384R. Malori haya yametengenezwa kwa ajili ya shughuli ngumu kama ujenzi, uchimbaji madini, na usafirishaji wa mizigo ya masafa marefu, huku yakihakikisha gharama za uendeshaji wa chini. 

Ali Timimi, Mkurugenzi Mtendaji wa CFAO Mobility Tanzania, alisisitiza dhamira ya kampuni hiyo katika kutoa suluhisho la usafirishaji linalotegemewa na ufanisi kwa biashara za Tanzania:

"Sekta ya usafirishaji wa kibiashara ni uti wa mgongo wa uchumi, ikisaidia sekta muhimu kama ujenzi, usafirishaji, na uzalishaji viwandani. CFAO Mobility Tanzania tunatambua changamoto wanazokutana nazo wafanyabiashara katika kupata malori ya gharama nafuu, yenye ufanisi wa mafuta, na utendaji wa hali ya juu. Malori ya Shacman yameundwa kuhimili mazingira magumu huku yakihakikisha gharama za uendeshaji zinapungua na faida inaongezeka. Kupitia huduma zetu bora za baada ya mauzo, tunawahakikishia wateja wetu huduma za uhakika na za kiwango cha juu. Nachukua fursa hii kuikaribisha rasmi Shacman kwenye familia yetu na kuwahakikishia wateja wetu wa malori kwamba hilli ni suluhisho wanaloweza kutegemea."

Shacman, kampuni iliyoanzishwa mwaka 1968 nchini China, imekua moja ya watengenezaji wakubwa wa malori mazito duniani, ikiwa na mfumo wa huduma wa kimataifa uliosimamiwa kwa viwango vya juu. Wei Yang, mwakilishi wa Shacman kutoka makao makuu ya China, alisisitiza dhamira ya chapa hiyo kwenye soko la Tanzania:

"Tanzania imekuwa moja ya masoko muhimu zaidi kwa Shacman, na tumejizatiti kuhakikisha tunatoa malori na huduma bora ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka. CFAO Mobility Tanzania ni macho na masikio yetu hapa nchini, na ninaamini wataweza kutusaidia kuelewa mahitaji ya wateja na kuhakikisha wanapata huduma bora."

Kwa kutazama sekta ya usafirishaji na uchukuzi inavyozidi kukua kwa kasi nchini Tanzania, uzinduzi wa malori ya Shacman ni hatua muhimu katika kuimarisha uwezo wa nchi katika usafirishaji wa viwandani na biashara. Ahadi ya CFAO Mobility Tanzania ya kutoa huduma bora na upatikanaji wa vipuri inahakikisha kuwa biashara za Tanzania zinapata mshirika wa muda mrefu wa kuaminika kwa mahitaji yao ya malori mazito.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...