Tuesday, March 4, 2025

DAS KAHAMA : WANAWAKE JITOKEZENI KUSHIRIKI MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI



Na. Paul Kasembo, MSALALA DC.

KATIBU Tawala Wilaya ya Kahama Bi. Glory Absalum amewasihi wanawake na wananchi wote wa kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani kwani watapata fursa ya kutembelea kwenye mabanda na kupata huduma mbalimbali za kijamii pamoja na kupata fursa ya kuuza na kununua bidhaa ikiwa ni sehemu ya kusherehekea juhudi za Serikali za kuimarisha haki usawa na uwezeshaji.

Ametoa wito huo leo Machi 4, 2025 wakati wa Uzinduzi wa Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayofanyika kwenye Kata ya Bugarama, Halmashauri ya Msalala Wilaya ya Kahama ambapo pia amesema Kaulimbiu ya mwaka huu inatoa mwaliko kwa watu wote kushiriki katika maadhimisho haya kuhakikisha kuna haki, usawa na uwezeshaji.

"Ninawasihi wanawake na wananchi wote kujitokeza kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake kwani mtapata fursa ya kutembelea kwenye mabanda na kupata huduma mbalimbali za kijamii ikiwa ni sehemu ya kusherehekea juhudi za Serikali za kuimarisha haki, usawa na uwezeshaji", amesema Bi. Glory.

AIdha amewasihi wanawake kuendelea kutumia nishati safi ya gesi kwa ajiri ya kupikia ili kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha kuna matumizi makubwa ya nishati safi yakiambatana na utunzaji salama wa mazingira.

Maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Duniani kwa Mkoa wa Shinyanga yanaadhimishwa kwa siku tatu kuanzia leo Machi 4 hadi Machi 6 katika Kata ya Bugarama, Halmashauri ya Msalala Wilaya ya Kahama yenye Kaulimbiu "Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji"

Source
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...