Wakili wa Mahakama Kuu, Fatma Karume, ameungana na mwanahabari Khalifa Said kwa kusema kuwa Chadema hakiwezi peke yake kuzuia uchaguzi mkuu ujao bila ushirikiano wa wananchi.
Kupitia ujumbe wake kwenye X, Fatma amesema kuwa suala kubwa si uwezo wa Chadema pekee bali ni uelewa na utayari wa wananchi kushiriki katika msimamo huo.
"Swali ni, wananchi wanaelewa kwanini Chadema wanasema hakuna maana ya kufanya uchaguzi katika mazingira haya?" alihoji.
Fatma alisisitiza kuwa kufanikisha msimamo wa "Hakuna Mageuzi, Hakuna Uchaguzi" kunahitaji zaidi ya kauli ya Chadema; kunahitaji uungwaji mkono wa wananchi kwa vitendo.
Aliuliza pia kama wananchi wako tayari kuzuia uchaguzi, akionyesha mashaka kuhusu uwezekano wa kufanikisha jambo hilo bila msukumo wa umma.
Kauli yake inakuja wakati ambapo mjadala unaendelea kuhusu iwapo Chadema kitatekeleza kwa vitendo msimamo wake wa kutoshiriki uchaguzi iwapo hakuna mageuzi ya msingi katika mfumo wa uchaguzi.
Wadau mbalimbali wa siasa wamehoji kama kweli Chadema kinao uwezo wa kulazimisha mabadiliko hayo au kama ni mkakati wa kisiasa tu.
Katika hali inayoendelea kuzua mijadala, bado haijafahamika iwapo wananchi wataunga mkono hatua za Chadema au kama chama hicho kitaweka mkakati mwingine wa kushiriki uchaguzi huku kikiendelea kupigania mageuzi ya kisiasa.