Tuesday, March 4, 2025

GCLA YASISITIZWA KUTOA ELIMU KWA WAJASIRIAMALI

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mh. Exaud Kigahe (kushoto), akisikiliza maelezo kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Bidhaa na Mazingira Dkt. Shimo Peter (kulia) akieleza kuhusu majukumu ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali katika Maonesho ya Viwanda na Biashara za Wanawake na Vijana Wajasiriamali Tanzania yanayofanyika katika viwanja vya Mlimani City jijini Dar es salaam, kuanzia Februari 27 hadi Machi 5,2025.

********************

Na Mwanaheri Jazza

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mh. Exaud Kigahe, ameitaka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuendelea kutoa elimu kwa Wajasiriamali ya namna bora ya matumizi sahihi na salama ya kemikali katika bidhaa wanazozalisha ili zisiweze kuleta madhara kwa jamii.

Naibu Waziri Kigahe ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati akifungua maonesho ya Viwanda na Biashara za Wanawake na Vijana Wajasiriamali Tanzania yaliyofanyika katika Viwanja vya Mlimani City jijini Dar es Salaam.

"Nichukue nafasi hii kuwashukuru sana TWCC kwa kuwaalika GCLA kuwa sehemu ya haya maonesho, kwa sababu kama mnavyojua kwenye bidhaa zetu za Viwanda nyingi zinatumia kemikali ambazo hazifai au kuzidisha ikawa hatari kwa afya za watanzania. Hivyo, jukumu lenu ni kuendelea kutoa elimu kwa wajasiriamali hawa ili wazalishe bidhaa zenye ubora lakini pia na usalama kwa walaji" alisema Naibu Waziri Kigahe.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Bidhaa na Mazingira Dkt. Shimo Peter, amesema utekelezaji wa utoaji elimu tayari unafanyika na wanaendelea kuwafikia wadau mbalimbali hapa nchini.

"Serikali kupitia Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali tumefungua Ofisi za Kanda na katika hizo Ofisi za Kanda sita pamoja na madawati kwenye baadhi ya mikoa tumekuwa tukitoa elimu kwa shughuli zetu zote tukiwashirikisha watoa huduma hao ambao ni wazalishaji wa bidhaa, kuwapa elimu kuhusiana na bidhaa wanazozalisha, kuhusiana na matumizi ya kemikali lakini pia huduma ya uchunguzi wa kimaabara ambapo tumekuwa tukichukua sampili zao na kuzipima katika maaabara zetu na kuwapa matokeo.

 Lakini pia na kuwapa elimu stahiki ili kuhakikisha kwamba bidhaa wanazozalisha zinakidhi viwango vya ubora wa ndani na nje hata kama wapo katika mikoa mbalimbali au pembezoni mwa mji. Kwa hiyo yote hii ni juhudi ya kuhakikisha kwamba elimu na huduma ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imefika katika maeneo yote hapa nchini". Alisema Dkt Shimo.


Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mh. Exaud Kigahe (kushoto), akitoa maelekezo kwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wakati alipotembelea banda la Mamlaka katika Maonesho ya Viwanda na Biashara za Wanawake na Vijana Wajasiriamali Tanzania yanayofanyika katika viwanja vya Mlimani City jijini Dar es salaam, kuanzia Februari 27 hadi Machi 5, 2025. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Bidhaa na Mazingira, Dkt. Shimo Peter.
Kaimu Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Bidhaa na Mazingira, Dkt. Shimo Peter (kulia), akitoa elimu kuhusu majukumu ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa mwananchi aliyetembelea banda la Mamlaka katika Maonesho ya Viwanda na Biashara za Wanawake na Vijana Wajasiriamali Tanzania yanayofanyika katika viwanja vya Mlimani City jijini Dar es salaam.
Mtumishi wa Mamlaka, Lulu Kiwia (kushoto), akitoa elimu kuhusu majukumu ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa mwananchi aliyetembelea banda la Mamlaka katika Maonesho ya Viwanda na Biashara za Wanawake na Vijana Wajasiriamali Tanzania yanayoendelea katika viwanja vya Mlimani City jijini Dar es salaam.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...