Na Baraka Messa, Mbozi
KUTOKANA na vitendo vya ukatili kukithir katika wilaya ya Mbozi mkoani Songwe Baraza la Madiwani Halmashauri hiyo limejipanga kupambana na janga hilo la ukatili vikiwemo vitendo vya ulawiti na ubakaji kwa watoto wadogo chini ya miaka nane.
Hayo yamebainishwa na katibu tawala wa Wilaya hiyo Mbwana Kambangwa akiongea na Habari Leo baada kikao cha baraza kamili la Madiwani kwa robo muhura mwaka 2023/2024 kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri hiyo ambapo amewataka madiwani kuongeza nguvu kwenye mapambano dhidi ya vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia katika maeneo yao.
"Matukio mengi ya ukatili kwa watoto wadogo yamekuwa yakiripotiwa na kuibuliwa na vyombo vya Habari mara kwa mara katika wilaya yetu ya Mbozi, hali hii imekuwa tishio kwa ustawi wa kizazi kijacho"
Amewataka madiwani ambao ni wawakilishi wa wananchi kujikita katika utoaji elimu mara kwa mara kuhusu madhara ya ukatili kwa watoto wadogo, ikiwa ni pamoja na kuwa karibu na watoto ili kubaini changamoto zinazowakabili ili wasaidiwe.
Kambangwa amesema pia wamepokea maelekezo kutoka Kwa Waziri Mkuu walipofanya kikao kupitia Mtandao ambapo kunamaagizo maalumu 13 walipewa ikiwemo la kupambana na ukatili wa Kijinsia huku akisema kuwa Mbozi ni miongoni mwa Wilaya zilizo kithiri kuwa na vitendo vya Ukatili wa kijinsia.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo George Msyani amesema Halmashauri inaendelea kupambana dhidi ya matendo ya kikatili huku mipango ikiwa juu ya kuendelea kutoa elimu Kwa jamii juu ya matendo ya Ukatili na kueleza athari zake.
" Tumepeana maagizo madiwani wote , suala la elimu ya ukatili katika kata zetu liwe ni ajenda ya kudumu, Kila diwani anapofanya mikutano atoe elimu kuhusu madhara ya ukatili kwa watoto wadogo tukishirikiane na watalaam wa ustawi wa jamii, maendeleo ya jamii pamoja na jeshi la polisi" alisema Msyani.
Kwa upande wake Neema Kibona alisema matendo ya Ukatili hasa Kwa Watoto wadogo yanazidi kushamili kutokana na uwepo wa kufichiana maovu kwa wanajamii hasa kwa kutaka kumaliza mambo kienyeji bila kufuata Sheria hali ambayo inaendelea kuwa changamoto kubwa.
Afisa elimu shule za msingi na awali wilaya ya Mbozi Dorothy Mwandila anasema ubize wa wazazi katika shughuli za kiuchumi kumekuwa na athari kubwa katika malezi ya watoto, kwani watoto wengi hulazimika kulelewa na watu wengine ambao sio wazazi na kupata madhara.
"Watoto wetu tuwalee wenyewe, tuache kuwategemea ndugu wengine na majirani kutulelea watoto wetu, kwa sababu matukio yaliyo mengi ya ulawiti na ubakaji kwa watoto chini ya miaka nane hufanywa na ndugu wa karibu,
Kuna madhara makubwa ya kutokuwa karibu na watoto, kuna kisa kimoja watoto wa mama mmoja baba mmoja kaka yao alikuwa anawaingilia kinyume na maumbile wadogo zake wawili chini ya miaka 10 bila wazazi wao kujua kutokana na ubize wa kuondoka asubuhi na kurudi usiku nyumbani" alisema Mwandila.
Program Jumuishi ya Taifa ya Malezi Makuzi na Maendeleo ya awali ya Mtoto iliyozinduliwa mwaka 2021, inayotekelezwa kwa miaka mitano yaani (2021/2022-2025/2026 inasisitiza wazazi ,walezi na jamii kuhakikisha wanawekeza kwa watoto kuanzia miaka 0-mpaka miaka 8 katika afua muhimu za lishe, afya , elimu, ulinzi na usalama pamoja na uchangamshi wa awali ili kufikia kikamilifu hatua za ukuaji.