Saudi Arabia itaanza kuwapokea wageni waliopata chanjo ya Covid-19 katika mji mtakatifu wa Kiislamu wa Makka ikiwa kama sehemu ya ibada ya hija ya umrah, ikiwa ni takribani miezi 18 baada ya mipaka yake kufungwa baada ya kuzuka janga la virusi vya corona.
Shirika la habari la Saudi limesema Wizara ya Hijja na Umrah imetangaza kuanza kupokea raia wa taifa hilo wenye nia ya kutaka kushiriki ibada ya Umrah, lakini pia kwa awamu watapokea maombi kutoka mataifa mbalimbali.
Aidha taarifa hiyo imeongeza kusema mamlaka zitaanza kukubali maombi ya kusafiri kuanzia kesho Jumatatu. Kwa hatua hiyo uwezo wa kupokea wageni katika mji ya Makka na Madia utaongezeka na kufikia watu milioni 2, kutoka 60,000.
Ibada ya Umrah ambayo kwa kawaida inafanyika katika kipindi chochote cha mwaka, ilifunguliwa tena Oktoba kwa mahujaji wa ndani, baada ya kufungwa kabisa kutokana na mripuko wa janga la corona.