Umoja wa Vijana wa CCM ( UVCCM) umekitaka chama chao kumchukulia hatua Mbunge wa Kawe, Josephat Gwajima kwa kitendo chake cha kuhamasisha watanzania wakatae chanjo ya Uviko-19.
Katibu Mkuu wa UVCCM, Kenani Kihongosi ameyasema hayo leo Jumanne Julai 28 2021 mara baada kumalizika kwa kikao cha sektarieti ya UVCCM.
Amesema mbunge huyo ametoa maneno ya kichochezi na kwamba yanakwenda kuwagawa wananchi kwa sababu Rais Samia Suluhu Hassan ameshatoa msimamo kwa wananchi wapate chanjo.
"Sisi umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi kauli zile tunazipinga na kuzilaani kwa sababu utaratibu wa CCM kama mbunge ana jambo lake anapeleka kwenye party cocus (kamati ya wabunge wa chama),"amesema.
Amesema utaratibu alioutumia mbunge huyo wakwenda kutoa maneno hayo kwa umma, kwamba mtu atakayediriki kuwaambia watu wachanjwe atakufa ni utovu wa kinidhamu.
"Lazima atambue yeye sio Mungu anayetoa uhai ni Mungu. Tunakiomba chama chetu viongozi wa namna hiyo aachukuliwe hatua kali za kinidhamu na ajieleze kwanini anaongea maneno ya namna hiyo,"amesema